Thursday 2 July 2015

Madereva wa treni wagoma.

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Zaidi ya madereva 100 wa treni ya Reli ya Kati, wameanzisha mgomo baridi kuanzia jana wakishinikiza madai yao mbalimbali kwa uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
 
Hali hiyo imeelezwa kuwa inahatarisha maisha ya mamia ya abiria wanaotumia usafiri huo kutokana na dereva mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, sasa kutumiwa kuendesha treni kwa muda mrefu.
 
Treni inayoendeshwa na mzee huyo mstaafu anayefanya kazi kwa mkataba, aliyefahamika kwa jina moja la Kisanga, iliondoka jana jijini Dar es Salaam kuelekea Mwanza na Kigoma.
 
Ilitarajiwa aendeshe treni hiyo mpaka Tabora, tofauti na utaratibu wa kawaida wa dereva mmoja kuendesha treni kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na kupokewa na mwingine.
 
Dereva anayepokea treni Morogoro hutakiwa kuendesha hadi Dodoma na mwingine huichukua hadi Tabora ambako madereva wa kuifikisha treni Kigoma na Mwanza huingia kazini.
 
Taarifa zilielezea jinsi Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ilivyojipanga kukabiliana na mgomo baridi huo wa madereva, kwamba ni kumuandaa Mkaguzi (Inspector) wa madereva hao, Zabron Kanuti, kupokea treni kwa Kisanga pindi itakapofika Tabora na kuifikisha Kigoma.
Treni iliyotakiwa kwenda jijini Mwanza, hadi kufikia jana saa 9:00 alasiri, haikuwa na dereva.
 
TRENI KUTOKA KIGOMA-DAR YAKWAMA MORO
Aidha, treni iliyokuwa inatoka Kigoma kwenda Dar es Salaam nayo ilikwama Morogoro kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa dereva aliyetakiwa kumalizia safari.
 
Treni iliyokwama Morogoro ni ile mpya inayofahamika kwa jina la Delux iliyotoka Kigoma kuelekea jijini Dar es Salaam, ilifika mjini Morogoro jana Saa 5:00 asubuhi lakini mpaka majira ya mchana haikuwa imeendelea na safari kutokana na kukosekana kwa dereva wa kuiendesha.
 
Taarifa za uhakika zilibainisha kuwa idadi kubwa ya madereva nchini kote hawapo kazini kutokana na sababu mbalimbali wengi wakitumia kisingizio cha kuumwa.
 
“Wengi wao wamepata vibali vya kupumzika kutoka kwa madaktari, ikielezwa kuwa wana matatizo kiafya lakini ukweli ni kwamba jamaa wanakatishwa tamaa na mazingira magumu kazini,” kilieleza chanzo muhimu cha habari.
 
SABABU ZA KUGOMA
Imeelezwa kuwa chanzo cha mgomo huo ni madereva hao kudai maslahi bora, usalama wa maisha yao, abiria na mizigo wanayosafirisha.
 
Kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), madereva wa treni wanatakiwa kupewa semina pindi TRL inaponunua kifaa wanachotumia kusafirishia abiria kama vile injini ya treni. Injini nane zilizotengenezwa nchini - 88XX na saba zilizotengenezwa Afrika Kusini - 90XX, zinatumiwa bila madereva kuwa na ujuzi nazo isipokuwa wanachofahamu ni kuziwezesha kwenda mbele na kurudi nyuma tu.
 
Chanzo kingine cha mgomo huo ni madai ya madereva kutofanyiwa kazi kwa miaka mingi licha ya kuyawasilisha kwa ngazi zote za utawala ikiwamo ngazi za wizarani.
 
Ilielezwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, sasa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, Septemba, 2014 baada ya kujiridhisha kuwapo kero hizo, aliagiza uongozi wa TRL kuzifanyia kazi lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
 
Malalamiko hayo ilielezwa kuwa yameishafikishwa hata ofisini kwa Waziri wa Uchukuzi wa sasa, Samuel Sitta, ambaye hata hivyo hajaanza kuyashughulikia.
 
Madai mengine ni ya ubovu wa nyumba (rest house), ambazo zimejengwa kwenye vituo vyote vikubwa vya treni kwa ajili ya madereva kuishi kwa muda wanaposafiri kikazi na kulazimika kuishi nje ya vituo vyao vya kazi.
 
Madereva wanalalamika kwamba nyumba hizo zina vitanda vyenye ukubwa sawa na vya wanafunzi (futi 3.5), magodoro chakavu na uchafu zikiwamo kunguni na pia vyakula wanavyopikiwa ni vibaya kutokana na waliopewa zabuni kudaiwa kuwa na uhusiano na ‘wakubwa’ hivyo kutohofia jambo lolote.
 
Kutokana na uchakavu huo, madereva hao wamekuwa wakidai walipwe posho ya kujikimu ambazo ni Sh. 45,000 kwa siku, moja ya madai ambayo hata hivyo, hayajatekelezwa tangu Juni, mwaka jana.
 
SITTA: SINA HABARI
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, alilieleza NIPASHE kwamba hakuwa hata na fununu ya mgomo huo, ingawa hawezi kuupuuzia. 
 
Alisema angefuatilia taarifa hizo kwa uongozi wa TRL na kuzitolea ufafanuzi ndani ya muda usiozidi dakika 45. Mwenyekiti wa Madereva, Christopher Mbalanga, alipohojiwa na NIPASHE kuhusu mgomo huo, hakuthibitisha wala kukanusha isipokuwa alisema ni mgonjwa hayupo kazini.
 

No comments:

Post a Comment