Thursday 2 July 2015

Lowassa: Mwenye ushahidi wa rushwa dhidi yangu ajitokeze

 Aeleze nilitoa lini, wapi, kwa nani.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema amechoshwa na tuhuma za kipuuzi za kumhusisha na rushwa na sasa amewataka wote wenye ushahidi wa tuhuma hizo dhidi yake wazitoe.
 
Akizungumza na mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mjini hapa jana alipokuwa akirejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho ili awanie urais kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, Lowassa alisema kwa muda mrefu kuna watu ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa rushwa tuhuma ambazo alisema siyo za kweli.
 
“Ninatoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi autoe. Aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua rushwa lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani,” alisema.
 
Aliongeza kuwa yeye ni muadilifu, na anaposema kuwa atasimamia vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu wala kumuonea haya yeyote.
 
“Ndugu wanachama wenzangu, na wananchi kwa ujumla, ni lazima sasa tufike mahali tuseme imetosha. Majungu yametosha, upotoshwaji umetosha, rushwa imetosha, na kwa pamoja tunaweza kukomesha haya. Tutayakomesha kwa kusimamia ukweli, uadilifu, uaminifu na kutenda kwa haki,” alisema Lowassa katika hotuba iliyovuta hisia kwa waliokuwa wanamsikiliza.

 Alisema tuhuma hizo zimeendelea hata wakati wa kutafuta wadhamini kwa baadhi ya watu kuzieneza.
 
“Tumefanya kazi ya kutafuta na kuomba udhamini kwa uadilifu na umakini mkubwa. Na hapa nitumie nafasi hii pia kuwashukuru makatibu na viongozi wote wa Chama katika mikoa na wilaya kwa maandalizi mazuri katika kuifanikisha zoezi hili,” alisisitiza.
 
Alisema kuwa walifanya kazi yao vizuri kinyume kabisa cha vijimaneno vilivyoenezwa kwamba kulikuwa na matumizi ya fedha katika kuwatafuta wadhamni.
 
“Hivi kweli, unahongaje watu zaidi ya laki nane?” alihoji.
 
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alisema tuhuma hizo zimekuwa zikitolewa na watu ambao wamekosa hoja na zinatolewa bila ushahidi wowote.
 
Aliwataka wote ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa miaka kadhaa sasa na kumhusisha na suala zima la rushwa, waache mara moja kwani hakuna hata chembe ya ukweli wa maneno hayo.
 
Alisema akifanikiwa kushika wadhifa wa urais, ataendesha nchi kwa kufuata katiba na sheria. 
 
Kuhusu safari ya kusaka wadhamini, Lowassa aliwashukuru wana-CCM waliomdhamini na kwamba walijitokeza kwa wingi jambo ambalo limempa picha ya kuungwa mkono na kukubalika.
 
Alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini walifanya hivyo kwa utashi wao na bila kishawishi chochote cha fedha au fadhila nyingine yoyote.
 
Alisema kuwa udhamini alioupata ni kielelezo cha vitendo kwamba wapo naye katika Safari ya Matumaini. 
 
“Nina matumaini na imani kubwa kwamba mtaendelea kuniunga mkono ndani ya Chamna chetu ili kwa pamoja na mshikamano ndani ya Chama niweze kuteuliwa kugombea kiti cha urais,” alisema.
 
Lowassa alisema: “Kwa mafanikio haya ya hatua ya awali nina imani kwamba ni ishara njema kueleke hatua zilizobakia na uweza wake Mwenyezi Mungu Mungu, na kwa ushirikiano wenu kwa pamoja tutalivuka daraja ili hatimaye niwatumikie kwa utumishi uliotukuka nikiwa Rais wa Awamu ya Tano.”
 
Aliongeza kuwa: “Nina shauku kubwa ya kuunganisha nguvu na uwezo ya kila Mtanzania katika kupambana na umasikini wa nchi hii. Umasikini wa watu wetu siyo amri ya Mwenyenzi Mungu. Nina imani kabisa kwa pamoja tunaweza kutumia rasilimali tulizo nazo kwa bidii, maarifa na ufanisi zaidi ili kutokomeza umasikini huu.”
 
Mbali na Lowassa jana makada wengine watano wa CCM walirejesha fomu ambao ni Luaga Mpina, Dk.Hamis Kingwangala, Mwigulu Nchemba, Dk. Hassy Kitine na Eldoforce Bilohe, hivyo kufanya waliorusisha fomu kufikia 33 kati ya 42 anasaka wadhamini ili wapate ridhaa ya Chama hicho kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge Oktoba 25, mwaka huu. (Soma kauli zao Ukurasa wa 8).
 
WENYEVITI 18 CCM WAMSINDIKIZA
Lowassa alisindikizwa na wenyeviti wa CCM katika mikoa 18, wabunge na wanasiasa wakongwe nchini akiwamo Kingunge Ngombale Mwiru na Paschal Ndejembi.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya Lowassa kurejesha fomu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma, alisema amemsindikiza Lowassa kwa hiyari yake na hajashawishiwa na mtu kutokana na kumuona ni mtu anayefaa kuwa mwenyekiti wa CCM Taifa.
 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa mjini kutoka Zanzibar, Boraafya Silima, alisema ameamua kuungana na Lowassa kutokana na hakuna mtu atakayeweza kukivusha chama hicho kilipo kwani yeye ni mtaji tosha ana nia na madhumuni ya kukiendeleza chama.
 
Naye Mwenyekiti wa CCM kutoka Mkoani Dar es salaam, Ramadhani Madabida, alisema Lowassa anauwezo wa kuliongoza Taifa na amedhaminiwa na watu wengi kutokana na kukubali utendaji wake.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti kutoka Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema utamaduni wa kusema kuwa wenyeviti wanamuunga mkono mtu yupi haujaanza leo bali umeanza  tangu zamani. 
 
“Hili suala la sisi kumuunga mkono mtu tunayemuona anafaa halijaanza leo bali limeanza kwa Kikwete hata kipindi ambacho Nyerere alikuwepo hivyo siyo geni, sisi wenyeviti pamoja na mgombea tunaamini mageuzi yatafanyika ndani ya chama,” alisema Mgeja.
 
Naye Kingunge, alisema anamuunga mkono Lowassa kutokana na kuwa ni chaguo la Watanzania.

No comments:

Post a Comment