Thursday 2 July 2015

Basi lagonga treni, wanne wafa, kujeruhi 33.

  Miongoni mwa waliokufa ni baba na mwanawe.
Basi la Fahisan Huwei, likiwa limeharibika baada ya kugonga treni ya abiria katika kijiji cha Kibaoni wilayani Kilosa jana.
Watu wanne, akiwamo baba na mtoto wake mwenye umri wa miaka sita, wamekufa papo hapo na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Fahisan Huwel,  walilokuwa wakisafiria kugonga treni la abiria mali ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) katika Kijiji cha Kibaoni wilayani hapa,  Mkoa wa Morogoro.
 
 Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa mkoa huo, Musa Malambo, ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 asubuhi, wakati basi hilo aina ya Isuzu Jouney  likitokea Kijiji cha Tindiga wilayani humo kwenda mjini Morogoro.
 
Malambo alisema basi hilo lilipofika katika eneo hilo, liligonga treni hilo lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kigoma kisha kupinduka mara mbili na kusababisha vifo hivyo na majeruhi hao.
 
Alitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva wa basi hilo lenye namba T837 CTN, Bakari Salehe Nyange, Mkazi wa Kilosa, kushindwa kuchukua hadhari alipofika kwenye eneo la makutano ya reli na barabara. 
 
Aliwataja waliokufa kuwa ni Sarehe Gomba (35), Mkazi wa kijiji cha Tindiga; Mama Husna (33),  wa Mamoyo; mtoto huyo Surati Mwajili (6) na baba yake aliyefahamika kwa jina moja na Mwajili (38),  wakazi wa Pugu jijini  Dar es Salaam .

 Alisema wanamshikilia dereva wa basi hilo ambaye ni mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, ambako amelazwa kwa matibabu.
 
 Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Dk. Dennis Ngaromba, amethibitisha kupokea maiti wanne na majeruhi hao, akisema baadhi ya wametibiwa na kuruhusiwa kutokana hospitalini kutokana na hali zao kuwa nzuri.
 
Alisema majeruhi watano hali zao mbaya kutokana na kujeruhiwa vibaya kifuani na kichwani huku wengine wakiwa hawana fahamu na kuwahamishia   Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.
 
Mmoja wa abiria wa basi hilo, Rajabu Abdallah,  alisema tangu walipoanza safari katika kijiji cha Tindiga,  dereva wa basi hilo alibadili njia ya kawaida ya Kibaoni, Mamoyo, Mabwegere na kupitia Kimamba na kwamba kutokana na mvua kunyesha, aliamua kutumia njia fupi ya Kipolelo yenye makutano na reli.
 
Alisema akiwa katika njia hiyo alikuwa kiendesha basi hilo kwa mwendo kasi bila ya kuchukua tahadhari ya alama kwenye makutano ya reli na barabara na kuligonha treni hilo.
 
Alisema baada ya kutokea ajali hiyo, dereva wa treni hilo lenye namba 8U03 , Ainea Chipindula,  Mkazi wa Morogoro, alisimama na kuwabeba majeruhi hadi Kilosa mjini kisha kukimbizwa hospitali ya wilaya hiyo kwa matibabu.

No comments:

Post a Comment