Monday 6 July 2015

Mbatia amshukia Spika Makinda.


Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia.

Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia,  amesema hakuna Spika aliyewahi kuonyesha udhaifu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyoonyesha Anna Makinda.
Amesema Makinda ameligawa vipande vipande Bunge la 10 na kutumiwa na mhimili wa utawala.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbatia alisema badala ya Bunge kuisimamia serikali, lakini Makinda ameshindwa kuliongoza Bunge hilo kutokana na shinikizo la mhimili wa utawala na kulazimika kufuata matakwa ya CCM na hivyo kuliongoza kwa ubabe.
 
Alisema tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha  Samuel Sitta na Pius Msekwa ambao walionyesha weledi na kuliongezea heshima Bunge, lakini Makinda ameriharibu kutokana na kuacha kusimamia Katiba ya nchi katika kuliongoza Bunge hilo.
 
“Siku zote mwanamke ndiye huwa ni mtu wa mwisho kuligawa Taifa, lakini limekuwa ni jambo la ajabu sana kuona mwanamke huyo ambaye angekuwa mstari wa mbele katika kuitetea nchi hii, lakini ameamua lifie mikononi mwake, hata bila kuficha ameonyesha wazi kwamba anatumika na serikali na CCM, Makinda yeye siyo kiranja wa bunge  ni mratibu tu,” alisema Mbatia.
 
Aliongeza: “ Badala ya Bunge kusimamia serikali kama Mhimili unaojitegemea, limejivua kazi yake na kuwa kiungo cha serikali na inalisimamia, na ndiyo  maana hata juzi mlisikia Serikali inasema imeoliongezea Bunge siku, badala ya Bunge lijiongezee lenyewe, hii ni fedheha.”
 
Mbatia alisema suala la kupelekwa bungeni kwa hati ya dharura na kujadiliwa miswaada mitatu ya mafuta na gesi ni ajenda ya siri ya kutaka kuiweka gesi kama dhamana ya CCM ya kupata fedha ya uchaguzi na  kwamba hicho ni kiashiria cha kuanza kuiuza nchi rejareja.
 
“Raslimali hizi badala ya kuwa neema kwa Watanzania, sasa inakuwa balaa, watu wachache wanataka kuwaibia Watanzania, hivi unawezaje kuwekaje miswaada hii muhimu kujadiliwa kwa pamoja na kuipeleka harakaharaka hivyo, sisi tumesema hatukubali kuona hujuma hizi zinafanyika dhidi ya rasilimali na Taifa,” alisema Mbatia.
 
Mbatia alisema msimamo wa Wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uko wazi, kwamba hawako tayari kujadiliwa miswaada hiyo kwa hati ya dharura na pia hawatashiriki wakati wa kuvunjwa bunge hilo Julai 9, mwaka huu.
Pia aliongeza kuwa hata wakiitwa katika meza ya maridhiano na Makinda hawatakuwa tayari kushiriki.
 
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kwamba chama hicho kina  ajenga ya siri ya kuifanya gesi kusaidia kuwa dhamana  katika uchaguzi, alijibu kwa kifupi kwamba ni uzushi.
 

No comments:

Post a Comment