Huku wajumbe wa muungano mkuu wa upinzani nchini Kenya-NASA, wakikongamano katika mji ulioko pwani ya nchi hiyo huko Mombasa, kumtafuta mgombea mkuu wa kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu nchini humo mwezi Agosti mwaka huu.
Waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Jenerali Joseph Nkaissery, ametoa onyo kali kwa muungano huo, ambao awali ulitangaza kuanzisha kituo mbadala, cha kupokea na kutangaza matokeo ya mwisho ya kura, katika uchagu mkuu utakaofanyika tarehe 8 Augosti mwaka huu.
Bw Nkaissery amesema kuwa kamwe hataruhusu mipango kama hiyo ifanyike, muda wote akiwa ndiye mkuu wa usalama wa ndani nchini Kenya.
Jenerali Nkaissery, ameeleza kuwa Tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya (IEBC), ndio taasisi kuu pekee yenye uwezo wa kusimamia shughuli zote za uchaguzi nchini humo, huku akiongeza kuwa, hakuna mtu, kituo, taasisi au kikundi chochote kilicho na uwezo wa kufanya hivyo, au kuwasilisha na kutangaza matokeo rasmi ya kura, kwani hilo linaweza kusababisha ghasia nchini.
Tangazo hilo la usalama limetolewa masaa 24 tu, baada ya ghasia kutokea mjini Kitengela kati ya wafuasi wa vyama vikuu vya kisiasa nchini humo- Jubilee, chake Rais Uhuru Kenyatta na ODM, cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga. Mji wa Kitengela upo kilomita 50 kusini mwa mji mkuu Nairobi.
Aidha waziri huyo wa usalama wa ndani nchini Kenya, alipongeza msimamo wa mwenyekiti wa tume hiyo ya Bw Wafula Chebukati, kwa kusimama kidete dhidi ya hatua ya muungano wa NASA, kuanzisha kituo mbadala cha uchaguzi mkuu, ambaye siku chache zilizopita alisema kuwa, katiba ya nchi hairuhusu jambo kama hilo kutendeka.
No comments:
Post a Comment