Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ameungana na wabunge katika kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti
Maalum (CHADEMA) Dkt. Elly Macha aliyefariki Machi, 31, 2017 katika
hospitali ya New Cross Wolverhampton nchini Uingereza.
Akizungumza katika tukio hilo
Waziri Mkuu ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai,
familia marehemu pamoja na wabunge wote.
Waziri Mkuu amesema enzi ya uhai
wake marehemu Dkt. Elly alitoa mchango mkubwa na ushauri mzuri katika
masuala ya elimu na uboreshaji wa maeneo ya watu wenye ulemavu.
Awali akisoma wasifu wa marehemu,
Mbunge wa Iringa Mjini, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa alisema Dkt.
Elly alipata ulemavu wa macho akiwa na umri wa miezi mitano baada ya
kuugua ugonjwa wa surua.
Mchungaji Msigwa alisema pamoja na
kuwa na ulemavu huo wa macho lakini haukuwahi kuwa kikwazo kwake kwani
aliweza kufanya jambo lolote lililokuwa ndani ya uwezo wake.
Mwili wa marehemu Dkt. Elly
umesafirishwa leo kwenda nyumbani kwake Usa River mkoani Arusha na
anatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha
Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Elly alizaliwa Juni 18, 1962
kwenye kijiji cha Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro, ambapo mbali na
wadhifa wa ubunge pia aliwahi kuwa Mshauri Mwelekezi wa Shirikisho la
Vyama vya Watu wenye Ulemavu vya Afrika Mashariki.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, APRILI 21, 2017.
No comments:
Post a Comment