Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeliagiza Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu
ya Maendeleo (United Nations Development Programs – UNDP) kwa upande wa
Tanzania kumuondoa nchini Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Awa Dabo.
Serikali ilifikia uamuzi huo
kutokana na Bi. Dabo kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya
Watumishi wenzake na Menejimenti ya Shirika hilo, hivyo kupelekea
kuzoretesha utendaji wa shirika hilo nchini na kupunguza kasi ya kuleta
maendeleo kwa Watanzania endapo hatua za haraka zisingechukuliwa.
Baada ya kuthibitishiwa kuondoka
nchini, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa rai kwa UNDP
kuwakumbusha Watumishi wake kuwa kipaumbele chao ni kufanya kazi na
Serikali ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya
Mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na Malengo ya Maendeleo
Endelevu ambayo yamefafanuliwa katika Agenda ya Mwaka 2030.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasilino ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 25 Aprili, 2017
No comments:
Post a Comment