Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amewaomba viongozi wa dini nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi na
walezi kuishi maisha yenye nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza
Mwenyezi Mungu na kusimamia malezi ya watoto na kuzingatia maadili ya
Taifa kwa ujumla.
“Tabia na mwenendo mzuri ni lazima
uanzie katika ngazi ya familia, mtaani na hatimaye katika jamii.
Tukirudia utamaduni wetu wa zamani wa kusimamia maadili kwa pamoja,
jamii yetu itanusurika kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumatatu, Aprili 24,2017) wakati akifungua kongamano kuhusu mmomonyoko
wa maadili na athari za dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya, lililofanyika mjini Dar es Salaam.
Amesema kila mzazi au mlezi
aone aibu, uchungu na ajutie anapoona mtoto yoyote akienda kinyume na
utaratibu wa kawaida wa maisha na ni vema wakatumia nafasi yao kwa
kuwahimiza vijana hao waishi maisha ya nidhamu na yenye kumpendeza
Mwenyezi Mungu.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali
ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga jamii yenye kuzingatia maadili
nchini na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli amekuwa akiwasisitizia
Watanzania wote kuzingatia maadili katika jamii kwa kufanya kazi kwa
bidii na kujiepusha na vitendo vyote vya rushwa na ubadhirifu.
Amesema maadili katika Taifa ni
moja ya tunu muhimu kwa kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo,
ujenzi wa umoja, amani, upendo, uvumilivu na mshikamano kwa jamii.
Amesema maadili ni nyenzo muhimu
sana katika ujenzi wa Taifa na huliepusha kuingia katika mifarakano na
migogoro. “Hivyo hatuna budi nasi kuyalinda maadili hayo kwa uwezo wetu
wote, ili tuyarithishe kwa vizazi vijavyo, kama vile sisi tulivyoyarithi
kutoka kwa waasisi wa Taifa letu,”.
“Hata hivyo, ninyi ni mashahidi
kuwa katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia vitendo vya mmomonyoko wa
maadili na matokeo yake yanaonekana dhahiri kama kuongezeka kwa vitendo
vya rushwa, kuiga tamaduni za nchi za kigeni ambazo sio njema na hazina
tija kwa jamii, na Taifa kwa ujumla”.
“Ni ukweli usiopingika kuwa
mmomonyoko wa maadili ni miongoni mwa vichocheo vinavyopelekea matumizi
ya dawa haramu za kulevya. Hivyo ni matarajio yangu kuwa mtaliangalia
kwa kina tatizo la mmomonyoko wa maadili ambalo kwa kiasi kikubwa
linatuathiri kama Taifa katika mipango ya Serikali na maendeleo ya Taifa
letu,” amesema.
Hivyo Waziri Mkuu amewapongeza
viongozi wa BAKWATA kwa kuwa na wazo la kufanya kongamano hilo lenye
kulenga kujadili namna ya kurejesha maadili katika jamii. Tukumbuke kuwa
Watanzania tutaendelea kuishi kwa upendo, amani na utulivu iwapo
tutazingatia maadili.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa
mapambano na vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inafanikiwa. Lengo ni
kuhakikisha kuwa waathirika wote wa matumizi ya dawa hizo wakiwemo
vijana, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa wanakombolewa dhidi ya janga
hilo.
Amesema Serikali itahakikisha
inashughulikia mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa
za kulevya bila ajizi, ambapo vyombo vyote vya kisheria vimeelekezwa
kushirikiana katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa ya kulevya kwa
kusimamia sheria ipasavyo.
Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka
ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Bw. Rogers Siyanga
amewaomba viongozi wa dini kuiunga mkono mamlaka hiyo kwa sababu
inafanya kazi kubwa ambayo inahitaji msaada wa watu wote.
Kwa upande wake Mufti na Sheikh
Mkuu wa Tanzania, Alhaji Abubakary Zuberi amesema viongozi wa dini
nchini wana jukumu la kukataza maovu na kuiamrisha jamii kufanya mambo
mema badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya kazi hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, APRILI 24, 2017.
No comments:
Post a Comment