Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
NMB, Bi. Ineke Bussemaker (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa
Jengo maalumu la kupumzikia wagonjwa wa nje na wasaidizi wao wanaokwenda
kupata huduma katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam. Kulia ni
Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi na Meneja wa Benki ya NMB
Kanda ya Dar es salaam na Pwani, Vick Bishubo (wa kwanza kulia)
wakifuatilia tukio hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
NMB, Bi. Ineke Bussemaker (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo
pichani) kabla ya kuzinduwa jengo maalumu la kupumzikia wagonjwa wa nje
na wasaidizi wao wanaokwenda kupata huduma katika Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Prof. Mohamed
Janabi akifuatilia mazungumzo hayo.
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB jana ilikabidhi Jengo
maalumu la kupumzikia wagonjwa wa nje na wasaidizi wao wanaowaleta
wagonjwa kupata huduma katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
ililopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi jengo hilo lenye uwezo
wa kuhifadhi watu 100 kwa pamoja wakiwa wamekaa kusubiri huduma,
Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi. Ineke Bussemaker alisema ujenzi wa jengo
hilo ni sehemu ya huduma za kijamii zinazoilenga sekta ya afya ambapo
benki hiyo imeweka utaratibu wa kusaidia.
Alisema kukamilika kwa jengo hilo
la kupumzikia kutasaidia wagonjwa wa nje na ndugu zao ambao hufika
kupata huduma JKCI kupumzika sehemu tulivu na salama huku wakisubiri
kuhudumiwa na madaktari wa kituo hicho bila kero. Alisema msaada huo NMB
inaamini imeutoa kwa wateja wao pia ambao nao hufika na kupata huduma
katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa
kukamilika kwa jengo hilo la kusubiria pia itatoa fursa kwa madaktari
kuwahudumia wagonjwa wao kwa ufasaha zaidi.
Aidha, Bi. Bussemaker aliongeza
kuwa Benki ya NMB kwa mwaka 2017 imepanga kutumia zaidi ya shilingi
bilioni moja kusaidia huduma za kijamii hususani katika sekta ya afya,
elimu pamoja na kusaidia majanga mengine yanayoikumba jamii. Kwa mwaka
2016 benki hiyo ilitumia takribani milioni 260 nchi nzima kusaidia vifaa
mbalimbali vya hospitalini huku jumla ya hospitali 33 zikinufaika kwa
msaada huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi
aliishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo na kudai hii sio mara ya kwanza
kwa benki hiyo kuisaidia JKCI katika shughuli zake. Alimpongeza msaada
huo ni mkubwa kwao na unajenga mazingira mazuri ya huduma kwa wateja wao
hivyo kuishukuru sana NMB pamoja na uongozi na wafanyakazi wake.
No comments:
Post a Comment