Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila mwanafamilia wa mpira wa miguu
Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za
shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.
Wanafamilia wa mpira wa miguu
ni pamoja na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi wa mpira wa ngazi
zote na waajiriwa wa taasisi ambazo ni wanachama wa TFF wa ngazi
mbalimbali.
Ili kutunza heshima ya mpira
wa miguu Tanzania, wanafamilia wa mchezo huo katika kutimiza masharti ya
kanuni za maadili za TFF, hawana budi kuheshimu na kufuata taratibu
zote hizo ndani na nje ya uwanja.
Taswira njema ya shirikisho
inajenga imani ya wadau wakiwamo serikali, mashirika mbalimbali ya umma
na binafsi, vyombo vya habari, vyama vya mpira vya kimataifa, NGO’s na
watu binafsi kwa taasisi (TFF). Kinyume chake ni kulibomoa shirikisho.
Dhima ya uongozi wa TFF ni
pamoja na kulinda na kutunza heshima hii. Hivyo vitendo vyovyote vyenye
viashiria vya uvunjaji wa maadili havitavumiliwa, na vikitokea hatua
zitachukulia.
Na kwa muktadha huu Shirikisho
la mpira wa miguu Tanzania, limemfungulia mashtaka ya kinidhamu Msemaji
wa Simba Bw. Hajji Manara kwenye Kamati ya Maadili. Leo hii Aprili 21,
2017 atapewa mashtaka yake na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa.
TFF inaendelea kutoa rai kwa
wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza,
kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya
mpira wetu.
No comments:
Post a Comment