Mwanariadha
Alphonce Simbu aliyeshika nafasi ya tano katika mashindano ya London
Marathon atembelea bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Leo Alhamisi
April 27 akiwa ni mgeni maalum wa Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na
Utamaduni Harison Mwakyembe. Baada ya kutembelea bunge hilo Simbu pia
atakuwa na mazungumzo na Waziri Mwakyembe.
Simbu ataambatana na muwakilishi wa wadhamini wake DStv pamoja na maafisa waandamizi wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT.
Akizungumzia mualiko huo,
mwanariadha huyo amesema kuwa amefurahi sana kupata mualiko wa Waziri
anayehusika na sekta ya michezo kwenda bungeni kama mgeni wake maalum.
Amesema hii inaonyesha kuwa serikali inatambua jitihada zake
anazozifanya katika kuiwakilisha vyema nchi katika mashindano ya
kimataifa. “Nimefurahi sana kualikwa na muheshimiwa Waziri kumtembelea
bungeni, bila shaka hii itakuwa fursa nzuri ya hata wabunge kutambua
jitihada tunazofanya vijana wao katika kuliletea taifa sifa. Natumaini
pia nitapata fursa ya kuongea ana kwa ana na Waziri” alisema Simbu na
kuongeza kuwa atatumia fursa hiyo kumueleza Waziri changamoto nyingi
wanazokabiliana nazo wanamichezo hapa nchini.
Amesema kuna mengi ya kuongea na
Waziri na kwamba anaamini mazungumzo yao yatakuwa na tija na manufaa si
kwake tu, bali kwa wanamichezo wote kwa ujumla.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano
wa Multichoice Tanzania Johnson Mshana, ambaye anaandamana na Simbu,
amesema kuwa anaamini kuwa ziara hiyo na mkutano na Waziri utakuwa na
manufaa makubwa kwani pia itakuwa ni fursa nzuri ya kujadili namna bora
zaidi ya Serikali kushirikiana na wadau katika kuimarisha na kuendeleza
michezo hapa nchini. “sisi kama wadhamini wa mwanariadha huyu tunaamini
kuwa kitendo cha Waziri kutualika ni ishara tosha kuwa kweli anadhamiria
kushirikiana na sisi wadau wa michezo ili kuongeza nguvu za pamoja za
kuimarisha michezo hapa nchini” alisema Mshana
Multichoice Tanzania kupitia DStv
imekuwa ikimdhamini Simbu tangu mwaka jana na udhamini huo pia
umewanufaisha wanariadha wengine ambao wamekuwa kambini kwa muda sasa
pamoja na simbu. “Kambi ya mazoezi ya Simbu ambayo ilidhaminiwa na DStv
pia ilikuwa na wanariadha wengine ambao wote walinufaika moja kwa moja
na udhamini huo. Tunaamini kuwa pia kati ya hao tutapata wanariadha
watakaofanya vizuri siku zijazo”.
Alphonce Simbu, ambaye pia ni
mshindi wa medali ya dhahabu katika mashindano ya Mumbai Marathon ni
miongoni mwa wanariadha wa timu ya Taifa itakayoshiriki katika
mashindano ya Dunia yatakayofanika jijini London mwezi Agosti mwaka uu
No comments:
Post a Comment