Wednesday, 12 April 2017

Serikali kufanya marekebisho katika Sheria ya ndoa ya Mwaka 1971

C7lLPt8V4AAjQlo
Na Daudi Manongi-MAELEZO, DODOMA.
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imesema inaendelea na mchakato wa ndani wa kufanyia marekebisho ya kuhuisha na kuimarisha maeneo yaliyo mazuri ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 na kuwasilishwa Bungeni ili kuendana na wakati.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Prof.Palamagamba Kabudi wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini Dodoma.
“Serikali inaendelea na mchakato huu wa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hii Bungeni ili iweze kuendana na wakati kwa kuondoa upungufu uliopo kwa maslahi mapana ya nchi yetu”,Aliongeza Mhe.Kabudi.
Amesema kuwa baada ya miaka 20 kupita tangu sharia hiyo ya ndoa itungwe,Serikali kupitia tume ya kurekebisha Sheria iliifanyia mapitio ya sheria hiyo na kubaini maeneo kadhaa yenye udhaifu na hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho.
Amebainisha kuwa  Kutokana na maoni hayo ya tume,mwaka 2008 Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria iliandaa waraka  wa baraza la Mawaziri uliokuwa na mapendekezo ya marekebisho ya sharia ya ndoa ya mwaka 1971,hata hivyo desemba 2010 kabla waraka huo kujadiliwa na kuridhiwa na baraza la Mawaziri mchakato wa mabadiliko ya katiba ya jamhuri ya muungano ukaanza na kulilazimu Baraza kusitisha kwa muda mchakato huo.
“Serikali ilikuwa na matarajio kuwa wakati tume ya mabadiliko ya katiba inakusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya katiba,wananchi wangetoa maoni kuhusu Sheria ya ndoa  pamoja na sheria  nyingine zinazofanana na hiyo na hivyo maoni yaliyotolewa wakati wa Sheria ya Ndoa yalikuwa machache sana”Alifafanua Mhe.Kabudi.
 
Sheria ya ndoa mwaka 1971 ni matokeo ya mjadala mpana na shirikishi kupitia waraka wa Serikali namba moja wa mwaka 1969.

No comments:

Post a Comment