Tanzania imeanza kuandaa kikosi
kipya cha timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 –
Serengeti Boys kitakachoshindana kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika kwa
vijana wenye umri wa chini ya miaka hiyo.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
barani Afrika (CAF), limeiteua Tanzania kuandaa fainali hizo mwaka 2019
hivyo sasa TFF imeanza kuandaa vijana wake.
Kwa kuanzia tu, imeanza kuwamulika vijana 22 wanaosoma Shule za Alliance zilizoko Mwanza.
Mapema wiki hii, ilimuagiza
Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu kwa Vijana, Kim Poulsen
kupima uwezo wa vijana hao kwa kufanya nao mazoezi kwenye viwanja vya
Alliance ambako amemaliza leo asubuhi na kusema: “Tuna timu bora ya
taifa.”
“2019 si tu kwamba Tanzania
itashiriki, bali kushindana. Lakini naipongeza TFF na Alliance kwa
kuanza program ya kuandaa timu bora. Serengeti Boys ya sasa inayomaliza
muda wake iliandaliwa kwa mwaka mkoja, lakini vijana hawa wenye umri wa
miaka 12 na 13 ni hazina nyingine kubwa kwa taifa…
“Kwa jinsi nilivyowaona itoshe
kusema tu tayari tuna timu. Nimesikia viongozi wa TFF wakisema kwamba
jicho lao si kwa vijana hawa tu, bali pia kwa vijana wengine Tanzania
nzima. Hili ni jambo zuri lenye manufaa mazuri,” amesema Poulsen
alipozungumza na waandishi wa habari leo mara baada ya mazoezi ya
asubuhi.
Nahodha wa timu hiyo ya vijana,
alishukuru Alliance kwa malezi mazuri na TFF kwa kuendelea kuwajali hasa
kwa sasa ambako nao wamesema ndoto zao ni kutaka kung’ara zaidi ya
Serengeti ya sasa ambao walitolewa na Congo Brazzaville katika harakati
za kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika,
zitakazofanyika mwakani nchini Madagascar.
Vijana waliotolewa kwa sasa
wanajipanga upya kwenda Korea Kusini kwa ajili ya kujiandaa na ratiba
mpya ya CAF na FIFA kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 ambako
timu ya taifa kwa hapa Tanzania inaitwa Ngorongoro Heroes. Ratiba za
michuano ijayo ya kimataifa, itatolewa baadaye mwaka huu.
No comments:
Post a Comment