Ni katika kukabiliana na ujio wa Serikali Dodoma
MENEJA wa Shirika la Ugavi wa
Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zakayo Temu amesema ni
vema mkoa huo ukapewa hadhi ya mkoa maalum ili uweze kukabiliana na
changamoto za ujio wa Serikali Dodoma.
Ametoa ombi hilo wakati akitoa taarifa ya utendaji wa TANESCO
Mkoa wa Dodoma mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alifika
kwenye kituo cha kupozea umeme cha Zuzu nje kidogo ya mji wa Dodoma,
kukagua mahitaji halisi ya umeme ikilinganishwa na ujio wa watumishi
mkoani humo.
Mhandisi Temu alisema: “Tunaomba
mkoa wetu wa Dodoma ambao ni Makao Makuu uangaliwe kwa jicho la pekee na
kupewa hadhi ya mkoa maalum kama ilivyo kwa Dar es Salaam ambako kuna
mikoa minne ya ki-TANESCO.”
“Dar es Salaam ina mikoa minne ya
Ilala, Kinondoni, Temeke na Mikocheni. Mkoa wetu unatakiwa kubeba
majukumu yote ya Serikali kama yanavyofanyika hivi sasa katika Jiji la
Dar es Salaam. Hivyo, tunaomba tupewe kipaumbele kwenye rasilmali watu,
usafiri na vitendea kazi,” alisema.
Alisema TANESCO inabidi iende kwa kasi zaidi ili kumudu wimbi la wafanyakazi wanaohamia Dodoma.
Akifafanua kuhusu uboreshaji wa
miundombinu iliyopo, Mhandisi Temu alisema kukamilika kwa njia ya
kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga kupitia
Dodoma, kumeboresha upatikanaji wa umeme kwenye mji wa Dodoma.
“Umeme unapatikana ukiwa na
voltage nzuri na hauchezichezi na hivi sasa tatizo la kukatika kwa umeme
mara kwa mara limepungua kwa kiasi kikubwa. Kukamilika kwa njia hii
kunaleta uwezekano wa kufanya matengenezo kwenye njia moja ya umeme bila
kuathiri upatikanaji wa umeme kama ilivyokuwa awali,” alisema.
Alisema kazi inayoendelea hivi
sasa ni kubadilisha nguzo za umeme zilizochakaa; kubadilisha njia za
msongo wa kilovolti 11 kwenda kilovolti 33 zenye urefu wa km. 85 na
transforma 74 ili kupunguza upotevu wa umeme na kuingiza njia hizo
kwenye njia mpya ya 132/33kV katika maeneo ya manispaa ambayo yanapata
umeme kupitia njia za 11kV.
Alisema mbali ya kusambaza umeme
kwa njia ya mzunguko wa mji (ring circuit), wataongeza vituo vikubwa
viwili vya kupozea umeme katika maeneo ya Msalato na Kikombo.
Mhandisi Temu alisema wameanza
kuboresha miundombinu ya umeme ili kuwezesha baadhi ya wilaya za
mipakani zipate umeme kutoka mikoa ya jirani wakati wa matengenezo au
kukiwa na hitilafu za umeme.
“Tunapanga wilaya ya Gairo ipate
umeme kutoka Morogoro; Bahi ipate umeme kutoka Manyoni; Mpwapwa hasa
maeneo ya Chipogolo yapate umeme kutoka Ruaha Mbuyuni ambako ni karibu
zaidi. Pia tunataka wilaya ya Kiteto ipate umeme kutoka Dodoma badala ya
Babati kama ilivyo hivi sasa,” alisema.
Alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba
umeme unaozalishwa na kituo cha Zuzu unatosha mahitaji ya sasa na hata
baadaye kwani wanazalisha megawati 48 wakati mahitaji ya juu ni megawati
25 na hivyo kubakiwa na ziada ya megawati 23.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa aliwaagiza viongozi wa TANESCO mkoa wa Dodoma wahakikishe
wanapeleka miundombinu ya umeme kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili
wanaonunua wakute huduma hiyo ipo tayari.
“Nimeongea na watu wa idara ya
maji, nimewaambia wapeleke miundombinu yao katika maeneo yanayopimwa
viwanja. Na ninyi pia mfanye hivyo kama ambavyo watu wa TAMISEMI
walijenga barabara za lami katika viwanja vipya vya makazi ili watu
wakienda kununua wakute huduma hiyo ipo tayari,” alisema.
“Nimefarijika kukuta kwamba
Dodoma hatuna shida ya umeme, hatuna mgao, kwa hiyo endelezeni kazi hii
nzuri mnayoifanya,” alisema Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment