Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara nchini (Tanroads), Eng. Patrick Mfugale(Wa kwanza kulia) akitoa
maelezo ya ramani ya Ujenzi wa barabara za maingiliono (Tazara Flyover)
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa(
Wa kwanza kushoto) wakati alipokagua ujenzi huo Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wa pili kushoto) akitoa maelekezo
kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Eng. Patrick
Mfugale (Kulia kwake) wakati alipokagua ujenzi wa barabara za
maingiliono (Tazara Flyover, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Katikati), akifafanua jambo mara
baada ya kukagua daraja la wapiti kwa miguu lilopo Buguruni Jijini Dar
es salaam. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini
(Tanroads), Eng. Patrick Mfugale na Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa
barabara wa Wizara Eng. Light Chobya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na Wananchi mara baada
ya kumaliza kukagua daraja la wapiti kwa miguu lililopo Buguruni Jijijni
Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Kampuni ya kikandarasi ya
Sumitomo Mitsui inayojenga mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover)
katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara
kumaliza ujenzi huo kwa wakati mradi huo ili kusaidia kupunguza tatizo
la msongamano.
Akizungumza mara baada kukagua
maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jijini Dar es salaam, Profesa Mbarawa
amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutajenga historia nchini
kutokana na kuwa ni wa mwanzo kujengwa.
“Nimefurahi kuona mradi huu upo
katika hatua nzuri, naomba mkamilishe mradi huu unakamilika kwa ubora na
kwa wakati ili tatizo la msongamano lililopo katika maeneo haya
kupungua au kuisha kabisa”, amesema Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa amemtaka
Mkandarasi kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa umakini na kwa uangalifu
wakati wa kipindi chote cha ujenzi ili kuitokuweza kusababisha foleni
katika eneo hilo.
Aidha, Waziri Mbarawa amewataka
wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi huyo ili
kurahisisha kazi za ujenzi huo kukamilika kwa wakati na kupata matokeo
chanya.
“Nawaomba watanzania wenzangu
kuwa wavumilivu na usumbufu wowote utakaojitokeza katika kipindi hiki
chote, kwani ukamilifu wa mradi huu utasaidia kupunguza tatizo la
msongamano katika barabara hizi”, amefafanua Waziri Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Profesa
Mbarawa amekagua daraja la watembea kwa miguu eneo la Buguruni Sheli na
kuwataka wananchi wa maeneo hayo kulitunza daraja hilo ambalo uwepo wake
umesaidia kupunguza ajali katika maeneo hayo.
“Ni matumaini yangu sasa wakazi
wa maeneo haya mtavuka kwa amani kupitia daraja hili, na ajali
zilizokuwa zikitokea maramara hazitakuwepo tena”’, amesema Profesa
Mbarawa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Patrick Mfugale amemuahidi
Waziri huyo kumaliza kwa wakati ujenzi huo na kumhaakikishia Waziri kuwa
ujenzi wa barabara hiyo utakuwa na viwango vilivyo bora.
Mradi wa Tazara Flyover ni msaada
kutoka Serikali ya Japan ambao umegharimu shilingi bilioni 93.4 na
unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2018.
No comments:
Post a Comment