Friday, 21 October 2016

Profesa Semboja: Wadau wa Habari toeni maoni yenu ili mboreshe Muswada wa Habari.

 index
Na Daudi Manongi,MAELEZO.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Haji Semboja amewataka wamiliki na wadau wa tasnia ya habari hapa nchini kuusoma na kuelewa madhumuni ya Muswada wa Huduma za Habari kwa ajili kusaidia maoni ambayo yataboresha muswada huo.
Profesa Semboja asema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi.
Amesema ni vema wanahabari na wadau wa habari wakausoma kwa kina na kutoa maoni yao kwani hakuna sababu ya kuuchelewesha muswada huo kwa ajili ya kuimarisha tasnia ya habari.
Profesa Semboja ameipongeza Serikali kwa kuwa na uwazi katika kuuleta muswada huu kwa jamii ili wauone na kuulewa na waweze kutoa maoni yao ili tupate kitu kilicho bora.
Amesema kuwa baadhi ya maeneo yaliyomo katika muswada huo yatasaidia wanahabari kuboresha taaluma yao na kuwa na wanahabari wanaotambulika.
Profesa Semboja amewataka wana habari kuusoma vyema muswada huo na kuacha kuwa na mawazo hasi huku akisisitiza ushiriki wao uwe mkubwa kwani muswada huu unapatikana kwenye mitandao na hivyo unamfikia mtu yeyote kwa urahisi kabisa.
Muswada wa Vyombo vya Habari ulichapishwa na kuwekwa hadharani tangu Septemba 2016, pamoja na mambo mengi mazuri wadau wakuu wote walishiriki katika hatua za ndani za serikali kutoa maoni na kwa sasa wanashiriki katika hatua ya Kamati ya Bunge.

No comments:

Post a Comment