Sunday, 23 October 2016

Kijiji cha Soga kata ya Soga wilayani Kibaha wamepewa mwezi mmoja kuhama kwenye shamba hilo ambalo limerudishwa mikononi mwa serikali.

unnamed-4
Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Kibaha, Tatu Selemani akielezea jambo kwa wananchi wa Soga, walioshiriki kwenye mkutano wa mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama wakati alipokwenda kuzungumza hatima ya wana Kazamoyo . 
 (Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Soga
WAKAZI zaidi ya 600 waliovamia shamba kwenye Kijiji cha Soga kata ya Soga wilayani Kibaha mkoani Pwani(KAZAMOYO)wamepewa mwezi mmoja kuhama kwenye shamba hilo ambalo limerudishwa mikononi mwa serikali.
Agizo hilo limekuja  baada ya aliyekuwa mmiliki wa shamba hilo Jangil Kasamal kunyanganywa kwa kushindwa kuliendeleza.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama ,alisema agizo hilo ni kuanzia mwezi huu hadi Novemba 18 
baada ya kutoa miezi miwili tangu agosti hadi oktoba mwaka huu kuwataka waondoke lakini hawakufanya hivyo.
Alitoa kauli hiyo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kwenye kijiji hicho.
Mshama alielezea kuwa watu hao hawako kisheria hivyo wanapaswa kuondoka ili shamba hilo lenye ukubwa wa hekari 900 litumike kwa shughuli nyingine za kijamii.
“Kamishna wa ardhi ameshatoa maelekezo juu ya shamba hilo kuwa baada ya hati ya umiliki kutenguliwa limerudishwa kwa halmashauri ambayo itaweka huduma za kijamii na si watu kujigawia kama wana Kazamoyo walivyofanya,” alisema Mshama.
Alisema wananchi hao ambao wengi wao wanatokea Jijini Dar es Salaam na kulipa jina eneo hilo kuwa Kazamoyo na kujiwekea uongozi wao ambao hauko kisheria kwa madai ya kushindwa kupatiwa huduma na uongozi wa kijiji cha Soga.
“Kutokana na hali halisi iliyopo na tangu mwanzo tulitoa maagizo muondoke kwani tayari wizara na vyombo husika vimeona kuwa taratibu za kukaa hapo zimekiukwa.
,” alisema Mshama.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Tatu Seleman alisema kuwa wamepata barua toka kwa waziri wa ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi ,Wiliamu Lukuvi ikisema kuwa watu hao wako hapo kinyume cha sheria.
Seleman alisema kuwa barua ya Waziri ilikuja baada ya wananchi hao kumwandikia barua wakitaka wamilikishwe eneo hilo ili wkae hapo kihalali.
Mmoja wa wakazi walioko kwenye eneo hilo alifafanua aliingia hapo baada ya kusikia eneo hilo linagawiwa ambalo lilikuwa shamba pori .
Awali Mery Kaijage alisema waliamua kuvamia shamba hilo na kugawana na kuanza kulima na kujenga kutokana na viongozi wa kijiji kuliuza eneo hilo kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment