Sunday, 23 October 2016

Ilichokisema Mahakama ya Makosa ya Jinai ICC kuhusu maamuzi ya Afrika Kusini

Baada ya kupata taarifa kuhusu nchi ya Afrika Kusini kuwasilisha barua yake Umoja wa Mataifa juu ya kujiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, Mahakama hiyo imeziomba nchi za Afrika Kusini na Burundi kufikiria upya uamuzi wao wa kuondoka katika mahakama hiyo iliyoundwa kwa lengo la shughulikia kesi za uhalifu mkubwa zaidi ulimwenguni.
Taarifa ya Rais wa mkutano wa vyama vya nchi wanachama waanzilishi wa mkataba wa ICC Sidiki Kaba amesema ingawa kujiondoa kutoka katika mkataba huo ni jambo huru, lakini anasikitika kwa maamuzi hayo na anaziomba Afrika Kusini na Burundi kufikiria upya maamuzi yao.
Aidha amezitaka nchi hizo kufanya kazi pamoja na mataifa mengine katika mapambano dhidi ya ukatili, ambao mara nyingi husababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kauli hii imekuja siku moja baada Afrika Kusini kuitangazia mahakama hiyo kuwa inafanya mchakato wa kujiondoa kutoka ICC baada ya Burundi kukamilisha suala hilo.
Afrika kusini imechukua uamuzi wa kuanzisha mchakato huo kufuatia kukumbwa na shinikizo mwaka uliopita kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, kuitaka imkamate Rais wa Sudan Omar al Bashir wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Johannesburg.

No comments:

Post a Comment