Monday 17 October 2016

Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke amemtembelea Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo jijini Dar es Salaam

uin1
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akielezea fursa za uwekezaji katika Sekta ya Nishati kwa Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto).
uin2
Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke akielezea mikakati ya nchi yake katika kuisaidia Tanzania katika  uboreshaji wa sekta ya nishati nchini.
uin3
Watendaji kutoka kutoka  Wizara ya Nishati na Madini,  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na   Wakala wa Ukaguzi wa Madini  Nchini (TMAA), wakifuatilia  maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
uin4
Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto) akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.
uin5
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akibadilishana mawazo na Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto) mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo ofisini kwake.
uin6
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke amemtembelea  Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo jijini Dar es Salaam  lengo likiwa ni  kujadili namna  Serikali ya  Uingereza inavyoweza kufanya kazi na  Tanzania kwenye uboreshaji wa sekta za Nishati na Madini.
Balozi Cooke alifanya mazungumzo na  Profesa Muhongo pamoja na Watendaji  kutoka  Wizara ya Nishati na Madini,  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na   Wakala wa Ukaguzi wa Madini  Nchini (TMAA)
Akielezea kuhusu Sekta  ya Nishati nchini, Profesa Muhongo alisema kuwa Serikali imeweka mikakati ya  matumizi ya  vyanzo vya nishati ya umeme kama vile  gesi,  maji, jotoardhi, makaa ya mawe, upepo, jua na kukaribisha wawekezaji kutoka  Uingereza kushirikiana na Serikali  kwenye uzalishaji na usambazaji wa umeme  nchini hususan  katika maeneo ya vijijini.
Aliongeza kuwa, Serikali imeanza  kutumia  gesi  yake  iliyogunduliwa kwa wingi kwa kiwango cha  futi za ujazo trilioni 57.2 kwa kujenga bomba la  gesi kutoka Mtwara hadi jijini  Dar es Salaam na kuendelea kusema kuwa  Serikali imeweka mkakati wa kusambaza gesi mikoani  pamoja na nyingine kuuzwa nje ya nchi.
“Kuna nchi  zilizopo Ukanda wa Afrika Mashariki zimeomba  bomba la gesi liende kwao; hii itatuwezesha sisi kufanya biashara pamoja nao na kuingiza  fedha za kigeni,” alisema Profesa Muhongo
Aliongeza kuwa, mikakati mingine inayofanywa na  Serikali ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kusindika  gesi kimiminika ( Liquefied Natural Gas Plant) na kiwanda cha mbolea katika eneo la  Kilwa mkoani Lindi na  kiwanda kingine cha mbolea katika mkoa wa Mtwara.
Alisisitiza kuwa, bado  Serikali inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini na kuomba kampuni za Uingereza zenye uzoefu kujitokeza na kuwekeza nchini.
Aidha, Profesa Muhongo alimwomba Balozi wa Uingereza kusaidia nchi ya Tanzania katika uendelezaji wa rasilimaliwatu kupitia  nafasi za ufadhili  zinazotolewa na ubalozi huo kwa ajili ya kusomea shahada ya uzamifu katika masuala ya  sheria na uzimamizi katika sekta za gesi na mafuta.
Naye,  balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke alisema serikali  yake inaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli  ya kufanya  Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kumhakikishia  Waziri, kuwa atashawishi  kampuni za Uingereza kuwekeza kwenye sekta za nishati na madini.

No comments:

Post a Comment