Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amevitaka vyuo vikuu Tanzania
kuunga mkono serikali ya Awamu ya Tano juu ya uanzishwaji wa viwanda
kuelekea uchumi wa kati.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo
leo katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua
maonyesho ya kumi na moja ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
yatakayofanyika kwa siku tatu kuanzia leo Julai 20 mpaka Julai 22 mwaka
huu.
“Vyuo vikuu vinatakiwa kuangalia
sera za nchi na mwelekeo wa Taifa kuelekea kukuza uchumi wa viwanda kwa
kuhakikisha wanatoa wataalamu ambao watashiriki katika uchumi wa viwanda
ambavyo vitaanzishwa nchini,” alifafanua Prof. Ndalichako
Prof. Ndalichako aliendelea kwa
kusema kuwa Serikali iko katika mkakati wa kuboresha vyuo vya ufundi kwa
kuanzia na vyuo vitatu vya ufundi vya Dar es Salaam, Arusha na Mbeya
ili kuboresha mafunzo wanayoyatoa kuendana na uhitaji uliopo katika
uanzishwaji wa viwanda.
Mbali na hayo, Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi inashirikiana na Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika uanzishwaji wa mafunzo katika
sekta adimu ikiwemo gesi kwa ajili ya kupata wataalamu watakaoajiriwa
katika viwanda vitakavyo anzishwa.
Vile vile wanafunzi wanaotarajia
kujiunga na vyuo vikuu hupewa maelekezo ya namna ya kuomba vyuo kupitia
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) pamoja na Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi (NACTE) katika maonyesho hayo.
Maonyesho ya Elimu ya Juu, Sayansi
na Teknolojia hufanyika kila mwaka yakiwa na Lengo la kutoa elimu kwa
wazazi na wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu hapa nchi waweze
kujua kozi zinazotolewa katika vyuo hivyo pamoja na maelezo ya kozi
hizo.
No comments:
Post a Comment