Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anaondoka nchini leo (Jumatatu, Mei 23, 2016) kwenda Lusaka, Zambia kuhudhuria Mkutano wa 51 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (51st Annual Meeting of the Board of Governors of the African Development Bank – AfDB) utakaofanyika kesho (Jumanne, Mei 24, 2016).
Na Chrispino Mpinge
Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli.
Mkutano huo ambao utafunguliwa na
Rais wa Zambia, Edgar Lungu utajadili masuala ya Nishati na Mabadiliko
ya TabiaNchi. Pia utahudhuriwa na Marais Idriss Deby wa Chad, Paul
Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya. Nigeria itawakilishwa na
Makamu wake wa Rais, Yemi Osinbajo huku Msumbiji ikiwazilishwa na Waziri
wake Mkuu, Carlos Agostinho do Rosário.
Watu maarufu waliothibitisha
kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Kofi Annan, Ashish Thakkar, John
Kufuor, Mary Robinson, Mo Ibrahim, Nancy Lee, Ngozi Okonjo-Iweala na
Tony Elumelu.
Mkutano huo utakaofanyika kwenye
kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mulungushi (Mulungushi
International Conference Centre) utahudhuriwa na washiriki zaidi ya
5,000 kutoka nchi 54 ambao ni wanachama wa benki hiyo, washiriki kutoka
nchi 26 ambazo si za bara la Afrika (non-regional member countries),
wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na wawakilishi
wa asasi za kiraia. Wengine ni Mawaziri wa fedha, biashara na uchumi na
wataalamu kutoka vyuo vikuu.
Waziri Mkuu amefuatana na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Asantu Kijaji, wachumi kadhaa pamoja na
wataalamu wa sekta ya fedha.
No comments:
Post a Comment