Na Mwamvita Mtanda
Serikali imefanikiwa kuwaunganisha Watanzania wanaotafuta kazi wapatao 20,000 ikiwa ni moja ya hatua ya kupunguza tatizo la ajira nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Msemai wa Wakala wa Huduma za Ajira nchini (TaESA) Bi Jamila Mbarouk wakati wa mkutano na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam.
Akizungumzia watafuta kazi
waliongushwa tangu kuanzishwa kwa wakala huo Jamila alisema kuwa wengi
waliounganishwa walikuwa wahasibu, Makatibu muhtasi, wataalamu wa huduma
za jamii.
“Jukumu letu letu ni
kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri ndani na nje ya nchi ili waweze
kupata huduma hii kwa urahisi kwa kuzingatia sheria na kanuni za Ajira
hapa nchini” alisisitiza Jamila.
Katika kupanua huduma ili
kuwafikia watanzania walio wengi Jamila amebainisha kuwa (TaESA)
imefungua ofisi za Kanda katika Mikoa ya Dodoma,Mwanza, na Arusha .
Mafanikio Mengine ni wakala
kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watafuta kazi 3185 ili kuweza
kuhimili ushindani na changamoto za soko la ajira.
Mafunzo hayo yametolewa
mbalimbali ikiwemo chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo cha Usimamizi
wa Fedha (IFM), Taasisi ya Uhasibu (TIA), Chuo cha Ardhi na Taasisi ya
Teknplojia Dar es salaam (DIT).
Akieleza Umuhimu wa mafunzo
hayo Jamila amesema kuwa yanalenga kuwajengea uwezo watafuta kazi ili
waweze kuandika barua za maombi ya ajira kwa ufasaha, kuandaa wasifu
binafsi (CV) na kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya mahojiano kwa
ufanisi kwa kuzingatia mbinu za kisasa.
Kwa upande wake Afisa Kazi wa
TaEsa Bw. Amani Kasale amesema kuwa baadhi ya watafuta kazi wamekuwa na
kasumba ya kuchagua maeneo ya kufanyia kazi hasa yale yaliyopo katika
miji mikuu hali inayozorotesha juhudi za Serikali kuwaunganisha watafuta
kazi na waajiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.
Akifafanua Kasale alisema kuwa
huduma ya kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri inatolewa bure kwa
watanzania wote wanaotafuta ajira kwa kuzingatia sheria na Kanuni za
ajira hapa nchini.
Pia Kasale alitoa wito kwa
vijana wote wanaotafuta ajira kuachana na kasumba ya kuchagua maeneo ya
kufanya kazi hasa yale yaliyo katika miji mikuu na kutumia fursa
zilizopo maeneo ya pembezoni.
Wakala wa huduma za Ajira
Tanzania TaESA Ulianzishwa kwa sheria ya wakala Na. 30 ya mwaka 1997
ikiwa na lengo la kuunganisha watafuta kazi na waajiri wenye fursa za
ajira ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment