Tuesday, 24 May 2016

Taasisi ya Mbalawala yaipongeza Nishati na Madini kuwezesha shughuli zake kufahamika

indexMeneja Uendeshaji   kutoka  Taasisi ya Wanawake ya Mbalawala Women Organization inayojishughulisha na uzalishaji wa briketi  za makaa ya  mawe wilayani Mbinga mkoani  Ruvuma, Hajiri Kapinga (kulia)  akielezea mafanikio ya  taasisi hiyo mara baada ya  taarifa zake kuanza kuchapishwa katika Jarida la  Wizara. Kushoto ni Kaimu Mkuu  wa Kitengo cha Mawasilano  Serikalini Wizara ya Nishati na Madini, Asteria Muhozya.
 

Na Kalonga Kasati 

Taasisi ya  Wanawake ya Mbalawala inayojishughulisha na  uzalishaji wa braketi za makaa ya mawe ijulikanayo kama Mbalawala Women Organization yanye makazi yake katika kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga mkoani  Ruvuma imeipongeza  Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikali kwa kutangaza shughuli zake hali iliyopelekea wateja wa makaa ya mawe katika taasisi hiyo kuongezeka kadri  siku zinazokwenda.

Taasisi hiyo inayofanya  shughuli zake karibu na Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka inajishughulisha na utengenezaji  wa briketi bora za makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia
Pongezi hizo zilitolewa na  Meneja Uendeshaji  wa Taasisi hiyo Hajiri Kapinga aliyekutana na  Kaimu Mkuu  wa Kitengo cha Mawasilano  Serikalini Wizara ya Nishati na Madini, Asteria Muhozya jijini  Dar es Salaam na kusema kuwa  tangu  Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kianze kuchapisha  habari zinazohusu  taasisi hiyo kupitia Jarida lake linalochapishwa kila wiki lijulikanano  kama MEM Newsbulletin  wameshuhudia idadi kubwa ya  wateja  ikiongezeka na  kuzidi  uzalishaji wa taasisi hiyo.
Alisema kabla ya  habari zake kuchapishwa na  Jarida la Wizara,  taasisi hiyo ilikuwa ikiwauzia briketi za  makaa ya mawe wateja wake  walioko katika  vijiji  vinavyozunguka mgodi wao  wilayani Mbinga mkoani  Ruvuma.

“Mara baada ya   taarifa zetu kuanza kuchapishwa na Jarida la  Wizara ya Nishati na Madini  tumeshuhudia mabadiliko makubwa kwani tumekuwa  tukipokea simu kutoka mikoa mbalimbali  hususan  Dar es Salaam,  Mbeya, Iringa wateja wakihitaji bidhaa,  hali inayopelekea  mahitaji kuwa makubwa kuliko  kiasi tunachozalisha,.” alisema Kapinga.
“Jarida limetufanya  tujulikane, hata wahisani wetu wameahidi kuongeza nguvu  na misaada katika kuwezesha  mradi huu  kuendelea vizuri; Jamii inasoma habari zetu na sisi tumesoma masuala mengi  kuhusu nishati na madini,” aliongeza

Kapinga aliendelea kusema kuwa ili kukabiliana na  mahitaji makubwa ya wateja taasisi hiyo imeweka mkakati wa kununua mtambo mwingine kutoka nje ya nchi  ili kuongeza uzalishaji utakaoendana na mahitaji ya wateja.

Alisema mikakati mingine ni pamoja na ujenzi wa ghala la kuhifadhia makaa ya mawe, ununuzi wa magari  kwa ajili ya usambazaji wa bidhaa ya briketi za makaa ya mawe katika  vituo vya uwakala  vitakavyoanzishwa nchini karibu kila mkoa.

“Mara baada ya kuanzisha vituo hivyo, wateja wetu watakuwa wanapata bidhaa  kutoka kwa mawakala badala ya kukutana na sisi moja kwa moja,” alisema Kapinga.
Alisema kuwa pia wamejipanga kutoa elimu ya matumizi ya briketi za matumizi ya makaa ya mawe na  utafutaji wa masoko  kwa kushirikiana na wadau wa utengenezaji wa majiko  sanifu yanayotumia briketi za makaa ya  mawe kwa matumizi ya majumbani.

Akielezea uanzishwaji wa taasisi hiyo, Kapinga alisema kuwa  taasisi hiyo  ilianzishwa chini ya ufadhili wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka (Tancoal Energy Limited)  unaomilikiwa na kampuni ya Intra Energy ya Australia kwa asilimia  70 na Serikali ya  Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo  la Taifa (NDC) kwa asilimia 30 ambao wanafurahishwa na   hatua iliyofikiwa na  taasisi hii  katika uzalishaji  ya briketi za makaa ya mawe.

Aliongeza sambamba na uzalishaji wa briketi za makaa ya mawe, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo juu  ya utumiaji wa briketi ya makaa ya mawe katika  vijiji na miji  jirani na mgodi wake pamoja na ushiriki katika maonesho mbalimbali ndani ya mkoa  wa Ruvuma.
“Lengo letu ni kuhakikisha briketi za makaa ya mawe zinazoendelea kuzalishwa katika mgodi wetu  zinatumika majumbani, shuleni , vyuoni na taasisi mbalimbali  na kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kutumia kuni” alisema Kapinga

Aliendelea kusema kuwa lengo la uanzishwaji wa taasisi hiyo lilikuwa ni  kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kupitia  briketi za makaa ya mawe na kuachana na matumizi ya kuni ambayo ni chanzo  cha uharibifu wa mazingira.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Asteria Muhozya alisema kuwa  lengo la  Jarida la Wizara ni kutangaza shughuli za nishati na madini  ikiwa ni pamoja na  taasisi zake
Muhozya aliongeza kuwa  jarida la Wizara  lipo  tayari kutangaza shughuli za wadau wa Madini  na Nishati ili kuhakikisha kuwa sekta  hizo zinakuwa na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi

No comments:

Post a Comment