Kila wiki serikali kupitia Wizara
yangu imekuwa ikitoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa
Kipindupindu nchini na hatua zinazochukuliwa kudhibiti ugonjwa huu. Hadi
kufikia tarehe 15 Mei 2016, jumla ya wagonjwa 21,477 wametolewa
taarifa, na kati ya hao 338 wamepoteza maisha.
Ingawa kwa ujumla wake kasi ya
ugonjwa wa kipindupindu imepungua ikilinganishwa na hali ilivyokuwa
mwaka jana, takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016
zinaonesha kuwa kasi ya ugonjwa imeongezeka kidogo ambapo idadi ya
wagonjwa wapya walioripotiwa wiki hiyo ni 212 ikilinganishwa na 138
walioripotiwa wiki iliyotangulia (Mei 2 hadi 8, 2016). Aidha, idadi ya
vifo vitokanavyo na kipindupindu pia imeongezeka katika wiki hiyo,
ambapo viliripotiwa vifo 5 ikilinganishwa na vifo 2 vya wiki
iliyotangulia. Wiki iliyoanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016, jumla ya mikoa
minane imeripoti ugonjwa wa kipindupindu. Mikoa hiyo ni Morogoro (78),
Lindi (51), Manyara (42), Dar es salaam (16), Mara (8), Pwani (8),
Kilimanjaro (6) na Kagera (3). Mikoa minne kati ya hiyo iliripoti vifo
vilivyotokana na
ugonjwa wa kipindupindu; Lindi (2), Morogoro (1), Mara
(1) na Kagera (1).
Halmashauri zilizoongoza kwa kuwa
na wagonjwa wengi katika wiki hiyo iliyopita ni Kilwa (51), Kilosa
(47), Babati Vijijini (33), Mvomero (23), Kinondoni (10), Mbulu (9),
Kibaha Mjini (8), Morogoro Mjini (8), Tarime Mjini (8), Same (6), Temeke
(6) na Bukoba Mjini (3). Halmashauri 4 ziliripoti vifo vilivyotokana na
ugonjwa huu; Kilwa (2), Mvomero (1), Tarime Mjini (1) na Bukoba Mjini
(1).
Kwa bahati nzuri, ugonjwa wa Kipindupindu hadi sasa haujaripotiwa kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma.
Takwimu hizi zinaashiria kuwa
ugonjwa wa kipindupindu bado upo katika jamii tunazoishi na unagharimu
maisha ya watu ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Hivyo wote kwa pamoja
hatuna budi kuendeleza juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa huu na
tuendelee kutekeleza na kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo
stahili inayotolewa na Wizara yangu.
Ni jambo la kusikitisha kwamba
bado tunashuhudia vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kipindupindu nchini,
ambavyo vingi hutokea katika jamii. Hivyo naomba nitoe wito maalum kwa
viongozi wa Vijiji/Mitaa na Kata, hasa katika maeneo yaliyoathirika,
washiriki kikamilifu kuhakikisha elimu sahihi ya huduma ya kwanza kwa
mgonjwa wa kipindupindu inatolewa katika maeneo yao kwa kushirikiana na
wataalam wa sekta ya afya katika ngazi hizo.
Napenda kuchukua fursa hii
kuwashukuru sana viongozi wa Mikoa na Halmashauri wanaosimamia kwa
ukamilifu upatikanaji wa takwimu sahihi za ugonjwa huu na kutoa wito
kuwa tuendelee na juhudi hizi za kutoa takwimu zenye usahihi na kwa
wakati ili kuweza kusaidia kuweka mikakati thabiti ya kutokomeza
kipindupindu. Aidha, Wizara inatoa rai kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kushirikiana na Viongozi wa Afya wa Mikoa na Wilaya katika kuhakikisha
takwimu hizi zinatolewa kwa usahihi na kwa wakati. Ni vema
tukakukumbushana kuwa ufichaji wa takwimu unachangia kwa kiasi kikubwa
kwa ugonjwa huu kusambaa kwa haraka na hivyo kushindwa kudhibitiwa kwa
wakati.
Wizara inasisitiza kuwa kwa
wakati huu ambao mvua za masika bado hazijamalizika, uwezekano wa
kuongezeka kwa ugonjwa wa kipindupindu ni mkubwa, na ni lazima tuongeze
juhudi za kuzuia maambukizi mapya. Kwa hiyo mikoa ambayo haina wagonjwa
ni lazima wachukue hatua za tahadhari ili kuzuia maambukizi mapya. Vile
vile, mikoa ambayo ina wagonjwa ni lazima iendelee kusimamia kikamilifu
hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huu.
Hivyo ni lazima wananchi
wazingatie kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira. Kama
tunavyoelekeza mara kwa mara kuwa ni marufuku kwa watu
kutitirisha maji taka ovyo, na pale hilo litakapofanyika
basi hatua za kisheria zichukuliwe na mamlaka husika. Aidha tunawasihi
viongozi mbalimbali wa ngazi zote; za vitongoji, vijiji, mitaa, kata na
tarafa kusimamia kikamilifu sheria ya Afya ya Mazingira hususan wakati
huu. Wizara inasisitiza kwa wananchi kutumia maji safi na salama
yaliyotakaswa kwa dawa kama vile waterguard au kuyachemsha ili kuepuka
kupata maambukizi ya kipindupindu.
Tunaendelea kuisihi jamii
kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za
kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia
yafuatayo:
- Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu.
- Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
- Mamlaka za maji zilizopo nchini zihakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
- Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu.
- Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
- Kutoa huduma ya kwanza katika ngazi ya jamii kwa mgonjwa yeyote mwenye dalili za kipindupindu kwa kumpatia ORS au maji yaliyochanganywa na chumvi na sukari.
- Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
- Watumishi wa afya kutoa takwimu sahihi na kamili za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa
wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika jitihada za
kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu. Aidha, Wizara
inaendelea kuwashukuru wataalamu
wa sekta mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na
Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwa
kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa
Kipindupindu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment