Simba SC wameshindwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara baada ya kuchapwa mabao 2-1 na wenyeji Kagera Sugar Uwanja wa
Kaitaba, Bukoba jioni ya leo.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ibaki na pointi zake 55 baada ya kucheza
mechi 25 na kuwaacha, mabingwa watetezi Yanga SC wakiendelea kuongoza
Ligi Kuu kwa pointi moja zaidi na Kagera Sugar inaendelea kukaa nafasi
ya tatu kwa pointi zake za mechi 25.
Katika mchezo huo uliochezeshwa Jimmy Fanuel, aliyesaidiwa na Joseph Masija wa Mwanza na
Geoffrey Msakila wa Geita,hadi mapumziko Kagera Sugar walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania,
Mbaraka Yussuf Abeid dakika ya 27 kwa shuti kali la umbali wa mita 22
baada ya pasi ya mchezaji mwenzake wa zamani wan Simba B, Edward
Christopher.
Simba wakaamua kufunguka baada ya bao hilo na kuanza kupeleka mashambulizi ya moja kwa moja langoni mwa Kagera Sugar.
Na Laudit Mavugo, Said Ndemla na Abdi Banda wote wakapoteza nafasi nzuri za kufunga wakiwa wamebaki na kipa Juma Kaseja.
Nafasi ambayo wataijutia zaidi Simba SC ni ya beki Banda dakika ya 43
ambaye alifanikiwa kuipata pasi nzuri ya beki wa kushoto Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’ na kuwatoka mabeki wawili wa Kagera Sugar, lakini
shuti lake dhaifu likadakwa na Kaseja aliyekuwa hatua mbili tu kutoka
kwake.
Kipindi cha pili, kila timu ilifanikiwa kupata bao moja, Kagera Sugar
wakianza kupitia kwa Edward Christopher aliyemalizia pasi ya Sulemani
Mangoma dakika ya 47 kabla ya Muzamil Yassin kuifungia Simba bao la
kufutia machozi dakika ya 67 akimalizia pasi ya Mghana, James Kotei.
Baada ya hapo, timu hizo zikaanza kushambuliana kwa zamu na sifa
zimuendee kipa mzoefu, Juma Kaseja aliyeokoa michomo kadhaa ya hatari ya
Simba.
Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Juma Kaseja, Godfrey Taita, Mwaita
Gereza, Juma Shemvuni, Mohamed Fakhi, George Kavila, Suleiman Mangoma,
Ame Ally ‘Zungu’/Ally Ramadhani, Edward Christopher/Themi Felix, Mbaraka
Yusuph na Japhet Makalai/Anthony Matogolo.
Simba leo kipo hivi; Simba SC; Daniel Agyei, Muzamil Yassin, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza
Kichuya/Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla/Juma Luizio, Laudit Mavuo, Ibrahim
Hajib/Mohammed Ibrahim na James Kotei.
No comments:
Post a Comment