Simba inashuka kuikabili Toto Africans ikiwa na morali ya juu baada ya juzi kushinda rufani yake na kupewa pointi tatu kutokana na Kagera Sugar kumchezea Mohammed Fakhi ambaye alikuwa na kadi tatu za njano kwenye mechi iliyowakutanisha Aprili 2 mwaka huu mjini Bukoba.
Omog amesema kuwa mechi ya leo dhidi ya Toto Africans ni zaidi ya fainali kwa sababu wanashuka kusaka pointi tatu ili kuendelea kujiimarisha kwenye mbio za kusaka ubingwa wa ligi hiyo, ikiwa inaongoza kwenye msimamo baada ya kufikisha pointi 61.
"Tulikuja kufanya kazi, kila mmoja amejipanga kukamilisha kazi, sina kingine cha kuongeza," amesema kwa kifupi kocha huyo wa zamani wa Azam FC.
"Tunashukuru Mungu tumepata pointi sita, kesho (leo) tutaingia kumaliza kazi iliyotuleta Mwanza, mechi ni ngumu kwa sababu Toto wanataka kujinasua wasishuke daraja na sisi tunawania ubingwa, " alisema nahodha wa Simba, Jonas Mkude.
Naye Kocha wa Toto, Fulgence Novatus, amesema mechi ya leo ni ngumu kwa kila timu kutokana na maandalizi yaliyofanyika na malengo ya kila klabu kuelekea mwisho wa msimu.
Simba itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 3-0 iliyoshinda katika mechi ya mzunguko wa kwanza lakini ikiwa haijapata ushindi kwa miaka saba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya wenyeji wake.
Mechi nyingine za ligi hiyo zinazotarajiwa kuchezwa leo ni kati ya Stand United dhidi ya Mtibwa Sugar (Kambarahe, Shinyanga), Ruvu Shooting ikiwakaribisha Majimaji na JKT Ruvu itakuwa wenyeji wa Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga.
No comments:
Post a Comment