Kenya inaingia kwenye kindumbwe ndumbwe cha Uchaguzi Mkuu, Agosti 8
mwaka huu na wagombea wanaotarajiwa kupambana vikali ni wale wale
waliotoana jasho kwenye uchaguzi wa mwaka 2013.
Hawa ni Raila Odinga aliyegombea kwa tiketi ya ODM wakati huo na Uhuru
Kenyatta aliyekuwa mgombea kupitia muungano wa vyama ulioitwa Jubelee.Kenyatta anatafuta kutawala muhula wa pili wakati Raila yeye anatamani kuikalia Ikulu ya Nairobi kwa mara ya kwanza.
Muungano wa upinzani safari hii umekuwa maarufu nchini Kenya kwa jina la NASA ama kwa kimombo ni National Supper Alliance.
Mpaka sasa muungano huo unaoundwa na vyama vya Amani, Ford Kenya, Wiper na ODM bado havijaamua nani apeperushe bendera ya muungano wao ingawa kuna uwezekano mkubwa Odinga akapitishwa.
Watu wanaowania urais ndani ya Muungano wa NASA ni pamoja na Kalonzo Musyoka wa Wiper, Raila Odinga wa ODM, Musalia Mudavadi wa Amani na Moses Wetangula wa Fork Kenya.
Uhuru Kenyatta ni nani hasa?
Kenyatta ni mtoto wa Rais wa kwanza wa taifa hilo ambaye aliingia katika siasa za Kenya alipoteuliwa kama mwenyekiti wa tawi la chama cha KANU kilichokuwa kinatawala mwaka 1997.
Rais mstaafu Daniel Moi alimuunga mkono sana na ilitokana na msukumo wake ndipo Uhuru aliingia katika siasa. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2003 aliwania urais na Mwai Kibaki lakini tofauti na matarajio ya wengi kuwa angeshinda alianguka.
Ni Daniel Moi aliyembeba Uhuru mpaka chama kikampitisha kuwania urais kwa tiketi ya KANU mwaka 2003, lakini aligundua kuwa ameshindwa vibaya kwenye uchaguzi huo alitangaza mapema kabla ya NEC ya Kenya kutangaza matokeo.
Uhuru alikerwa sana na kuanguka kwenye nafasi ya urais na mwishowe aliahidi kuwa hatajihusisha na masuala ya kisiasa kwa muda.
Tangu mwanzoni watu wengi waliona namna alivyokuwa akimbeba Uhuru kuwa ni kumtayarisha kwa mambo makubwa katika siku za baadaye kama alivyombeba kuwania urais.
Aliposhindwa mara moja alirejea katika biashara za familia yake ambazo zinajumuisha hoteli tano mashuhuri, kampuni za vifaa vya ndege na kilimo cha biashara. Lakini hakujua kuwa Moi bado alikuwa na mpango naye kutaka kumpeleka katika ngazi za juu.
1999 Rais Daniel Arap Moi alimpa Uhuru nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii na aliendelea kumpandisha ngazi kwa kumpa nafasi ya mbunge mteule na kumfanya Naibu Waziri.
Mwaka 2002 Moi akambeba tena Uhuru na kumpachika kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa KANU na kuanzia hapo chama hicho kikaanza kugawanyika huku vigogo wa chama hicho wakijondoa kwenye chama.
Tangu alipoingia katika mikono ya Moi, Uhuru alikuwa akitaka kuonyesha watu kuwa yeye anaweza kujitegmea wala siyo kibaraka cha Moi kama wengi walivyokuwa wanasema.
Baadaye alimshinda kigogo wa chama cha KANU Nicholas Biwot walipogombea uenyekiti wa chama hicho
Mgombea wa urais 2002
Julai mwaka 2002 ilionekana wazi kwamba Moi alimtaka Uhuru awe mgombea wa urais kwa tiketi ya KANU na alipenda awe ndiye mtu atakayemrithi Ikulu.
Mkutano Mkuu wa KANU uliofanyika mwezi wa Oktoba 2002 uliitikia mapenzi ya rais ukamtangaza Uhuru kama mgombea wa urais.
Hatua hiyo iliwakera wanasiasa wengi wasiokuwa Wakikuyu na waliondoka katika KANU na kuendelea katika ushirikiano wa upinzani wa NARC. Aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mwai Kibaki naye aliondokea kwenye mkumbo huo.
Uhuru kama kiongozi wa upinzani
Katika Bunge jipya alikuwa kiongozi wa upinzani lakini aliona pia upinzani ndani ya chama hasa kutoka kwa Nicholas Biwott pamoja na wanasiasa kutoka Bonde la Ufa.
Kwenye mkutano wa chama wa Januari 2005 Uhuru alithibitishwa kwa kura nyingi na hapo Biwott akaondoka kwenye na kuunda chama chake cha New Kanu.
Upingamizi dhidi yake ndani ya KANU
Katika kura maalumu ya wananchi kuhusu katiba mpya, Uhuru alishikamana na viongozi wengine katika kambi ya machungwa.
Mipango yake ya kushiriki katika Orange Democratic Movement(ODM) yalipingwa vikali ndani ya chama kwa sababu wana KANU pamoja na rais mstaafu Moi waliogopa kupotea kwa chama cha kwanza katika historia ya Kenya.
Novemba 2006 Biwott alirudia jaribio la kumpindua Uhuru kwa kuita mkutano wa Kanu mjini Mombasa bila idhini ya mwenyekiti wala kamati ya chama.
Hapa alichaguliwa kuwa mweyekiti mpya. Kwa msaada wa serikali Biwott alifaulu kuandikisha kamati yake kama uongozi rasmi hivyo kumwondoa Uhuru katika nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni.
Kuhamia upande wa Kibaki 2007
Juni 2007 Uhuru alionyesha wazi kwamba alitaka kuacha ushirikiano wa ODM kwa kutopeleka jina lake kati ya wagombea wa urais upande wa ODM. Badala yake alieleza ya kuwa atampigania Rais Kibaki achaguliwe tena. Alisema hana nia ya kugombea urais ikiwa hana uhakika kuwa atashinda.
Kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata, Kibaki alitawazwa kama rais licha ya utata huo. Kibaki naye alimteua Uhuru kama Waziri wa Serikali za Mitaa na baada ya mapatano kati ya Kibaki na Odinga, Uhuru aliteuliwa kama Naibu Waziri Mkuu ikiwa ni sehemu ya kugawana mamlaka.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2013 Uhuru alichaguliwa kama rais baada ya kumshinda mpinzani wake Raila Odinga kwa idadi ya kura za urais na kupata asilimia 50.3, kama inavyohitajika kwenye Katiba mpya.
Raila Odinga ni nani hasa katika siasa za Kenya?
Raila Odinga anatoka kabila la Luo, ambalo ni kabila kubwa la tatu nchini Kenya. Alizaliwa mjini Maseno, wilaya ya Kisumu, mkoa wa Nyanza, 7. 1. 1945.
Alikuwa mtoto wa pili wa wazazi wake. Baba yake aliitwa Oginga Odinga na mamake aliitwa Mary. Kuna watu maskini wengi nchini Kenya lakini familia yake hawakuwa maskini, bali walikuwa na mali, na hasa sasa wana mali.
Jambo hilo ni muhimu kwa sababu ikiwa mtu anataka kufanya siasa ni lazima kuwa tajiri.
Baba wa Raila, yaani Oginga, alikuwa mtu maarufu wa Kenya. Alikuwa kiongozi wa kabila la Luo na aliitwa “Ker”. Neno hili lina maana ya kiongozi wa kiroho, na kwa sababu kabla ya Oginga, Ramogi Ajwang alikuwa Ker, Oginga aliitwa Jaramogi pia.
Katika mwaka wa elfu moja mia tisa hamsini na saba, Oginga aliacha hadhi ya Ker na alikuwa kiongozi wa kisiasa wa Wajaluo.
Mwaka wa elfu moja mia tisa na sitini Oginga, pamoja na Tom Mboya, mtu mwingine wa kabila la Luo, walianza chama cha siasa kilichoitwa KANU.
Ingawa Oginga alikuwa kiongozi wa Luo na Mboya alikuwa mluo pia, Mboya alipendwa na watu wa Kenya zaidi. Labda Mboya angekuwa rais wa Kenya wa kwanza, lakini kwa sababu Oginga hakutaka mtu mwingine wa Luo kuwa rais alimuunga mkono Jomo Kenyatta kuwa rais wa Kenya wa kwanza.
Kwa hivyo rais wa kwanza wa Kenya alitoka kabila la Kikuyu na tangu wakati huo mpaka sasa kabila la Luo hawana nguvu ya kisiasa sana katika Kenya. Bali makabila mengine, yasiyopenda Luo wanatawala. Kwa hivyo itakuwa vigumu kwa mjaluo kuwa rais wa Kenya.
Baada ya kumuunga mkono Kenyatta, Oginga alikuwa kaimu wa rais wa kwanza nchini Kenya. Lakini kulikuwa na mgogoro kati ya Oginga na Kenyatta. Oginga alisema vitu vibaya vingi kuhusu sera za Kenyatta.
Halafu, mwaka 1966 aling'atuka, akatoka KANU, na akaanza chama cha KPU.
Kwa sababu ya vitu ambavyo Oginga alifanya, na kwa sababu Oginga alikuwa mtu wa serikali, Raila Odinga alipokua alifikiri juu ya siasa sana.
Lakini hakuanza kufanya siasa hadi takriban mwaka 1980 baada ya kumaliza elimu yake. Kwa hivyo, kwa vile tunajua kuhusu familia ya Raila Odinga, sasa tutajadili elimu yake halafu hatimaye siasa yake.
Elimu
Raila Odinga alisoma sana, na alikuwa mwanafunzi mkali. Kwanza alisoma katika shule ya msingi ya Kisumu Union. Baadaye alienda Maranda Sekondari. Shule zote zilikuwa katika mkoa wa Nyanza.
Lakini hakumaliza sekondari katika shule ya Maranda bali alitoka Kenya akaenda nchi ya Ujerumani. Alimaliza sekondari katika shule ya Herder Institute. Baada ya sekondari alienda chuo kikuu cha Otto von Guericke, mjini Magdeburg huko Ujerumani.
Hii ni shule ya sayansi, hasa uhandisi. Raila alisoma katika kitivo cha uhandisi mitambo (Mechanical Engineering). Alipata shahada mbili katika shughuli hii. Baadaye alirudi nchini Kenya.
Raila ana famÃlia ambayo si kubwa sana, lakini si ndogo pia. Mke wake anaitwa Ida. Wana watoto wanne, wanawake wawili na wanaume wawili.
Mtoto wa kwanza ni mwanaume anayeitwa Fidel ambaye anafanya biashara. Rosemary ni mtoto wa pili na aliolewa na Amos Akatsa na Rosemary anasaidia watu wanaotumia kompyuta. Raila Jr. ni mwanaye mwingine. Yeye anafanya kazi katika benki.
Mtoto kitinda mimba anaitwa Winnie. Kama Odinga atapitishwa na muungano wa vyama ujulikanao kama NASA basi atatoa changamoto kubwa kwa uhuru ambaye pia walirarurana kwenye uchaguzi kama huo mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment