Na Ally Daud- MAELEZO
Serikali kupitia mpango wa Taifa
Wa kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele itaanza kugawa
kingatiba za ugonjwa Wa matende, mabusha na Minyoo Oktoba 25 mwaka huu
ili kuondoa kabisa magonjwa hayo mpaka ifikapo 2020.
Akizungumza hayo katika semina na
waandishi Wa habari kuhusu magonjwa hayo Afisa Mpango wa huduma hiyo
Bw. Oscar Kaitaba amesema kuwa zoezi hilo litaanza Oktoba 25 hadi
Oktoba 30 mwaka huu katika maeneo yote ya Dar es salaam.
“Zoezi la kugawa kingatiba kwa
wananchi Wa Dar es salaam litaanza Oktoba 25 na kumalizika Oktoba 30 ili
kuweza kupambana na vimelea vya magonjwa hayo na kuendelea na mikoa
mingine” alisema Kaitaba.
Aidha Bw.Kaitaba amesema kuwa
kingatiba ambazo zitatolewa ni Ivermectin na Albendazole ili kuondoa
magonjwa ya Matende,Mabusha, na Minyoo kwa wakazi wa Dar es salaam na
vitongoji vyake .
Bw.Kaitaba amesema kuwa kingatiba
hizo zitatolewa kwa wananchi wote wenye umri kuanzia miaka mitano na
kuendelea katika maeneo yote ya Dar es salaam katika stendi za mabasi,
Masoko,Hospitalini, Ofisi za Serikali za Mitaa, Ofisi za Wizara, Kambi
za majeshi ns Magereza.
Aidha Bw.Kaitaba ameongeza kuwa
wananchi wanatakiwa wajitokeze kwa wingi kupata kingatiba hizo wakiwa
wameshakula vizuri chakula na kuondokewa na imani potofu kwamba
zinachangia kuzuia mimba ama kwa wanaume kupungukiwa nguvu za kiume.
Kwa upande wake Muhamasishaji Wa
Mpango huo kutoka Wizara ya Afya Bw. Makora Said amesema kuwa Semina
hiyo inahusu kuwahamasisha waandishi wa habari kutoa elimu kwa wananchi
kuhusu Mpango Wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele nchini kama vile Matende, Mabusha, Minyoo, Usubi, Trakoma na
Kichocho.
Aidha Bw. Makora amesema kuwa
kama waandishi watakavyoielimisha jamii kwa elimu ya kutosha na wananchi
wakakubali wito Wa kutumia kinga tiba hizo Serikali itafanikiwa
kuepusha ulemavu na udumavu kwa watanzania.
Aidha Bw. Makora amesema kuwa
waandishi wanatakiwa wawe kipaumbele katika kuandika habari za afya ya
Binadamu ili kuwapa ufahamu wananchi na uwezo Wa wa kufanya maamuzi
sahihi juu ya afya zao kwa ujumla.
Semina hiyo ya siku moja imelenga
kuwaelimisha waandishi Wa habari kuhusiana na Mpango Wa Kudhibiti
magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ili elimu ya kutosha ikatolewe
kwa wananchi ili kufanikisha lengo la Sera ya Afya ya mwaka 2007 hadi
kufikia 2020.
No comments:
Post a Comment