Hussein Makame, NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imevitaka vyombo vya habari kuialika tume hiyo iwapatie elimu ya mpiga
kura ili kukuza uelewa wa vyombo hivyo juu ya sheria, kanuni, na
taratibu zinazoongoza uchaguzi na kufahamu majukumu ya tume hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani wakati akieleza tathmini yake
juu ya elimu ya mpiga kura inayotolewa na tume hiyo ofisini kwake jijini
Dar es Salaam hivi karibuni.
Alisema NEC imejipanga kutoa
elimu ya mpiga kura nchi nzima na iko tayari kupokea maombi ya kwenda
kutoa elimu hiyo kwa wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na
wafanyakazi wote wa vyombo hivyo ili kukuza uelewa wa sekta hiyo.
“Niwaombe vyombo vya habari,
tumeanzisha programu ya elimu ya mpiga kura tualikeni kwenye vyombo
vyenu vya habari, mtualike tuje tuzungumze na nyinyi vyombo vya habari
kimoja baada ya kingine” alisema Bw. Kailima na kufafanua kuwa:
“Sisi tunataka kuzungumza na wewe
mmiliki wa chombo na watumishi wako na viongozi wenzako wote ili
tukueleweshe kuhusu Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya
Serikali za Mitaa, utaratibu mzima wa uchaguzi na uijue Tume ili
unapoandika ujue ninachoandika si cha kubahatisha”
Bw. Kailima alisema elimu hiyo
kwa vyombo vya habari pia itaviwezesha kuwa na uelewa mpana juu ya
masuala mbalimbali ya uchaguzi na kutoa changamoto kwa mtendaji huyo wa
NEC pindi anapopata na nafasi ya kuzungumza nao.
Katika kutekeleza mkakati
endelevu wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, Bw. Kailima ameanza
kutoa elimu hiyo kupitia televisheni mbalimbali nchini na kwamba yuko
tayari kuzungumza na vyombo mbalimbali kutekeleza mkakati huo.
Kwa upande mwingine, Bw. Kailima
amewataka Watanzania wakisikia kuna maonesho au mkutano ambapo Tume
inashiriki wafike banda la NEC waulize maswali wapate ufahamu na
watapata uelewa mkubwa juu ya mchakato wa uchaguzi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti,
Bw. Kailima alisema NEC itahakikisha inatumia maonesho, mikutano na
mikusanyiko mbalimbali ikiwemo mikutano ya kidini ili kutoa elimu ya
mpiga kura ikiwemo shule za sekondari nchini.
Alisema lengo kuu la kutekeleza
hayo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 wananchi wawe wamepata uelewa wa
kutoa kuhusu taratibu za uchaguzi na kufahamu majukumu ya Tume ili
kupunguza malalamiko na upotoshaji unaofanywa katika kipindi cha
uchaguzi.
Tayari Bw. Kailima ameshatoa
elimu ya mpiga kura kupitia televisheni za Shirika la Utangazaji la
Zanzibar (ZBC) na Televisheni ya Afrika Mashariki (EATV) na amesema NEC
inajipanga kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii.
Alisema aidha NEC itatoa
matangazo kwenye vyombo vya habari kuziomba Asasi za Kiraia zinazoweza
kutoa elimu ya mpiga kura kutuma maombi ili kupatiwa ridhaa ya kutoa
elimu hiyo kwa umma.
No comments:
Post a Comment