Na Daudi Manongi-MAELEZO
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL)
imetoa ofa ya mwezi mmoja kwa abira wanaosafiri kutoka Dar es salaam
kwenda Mwanza kulipa nauli ya shilingi 160,000/- kwa safari moja.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es salaam na na Kaimu Afisa Mawasiliano wa Kampuni Bi.Lily
Fungamtama wakati akiongea na Idara ya Habari.
Amesema Ndege za Kampuni zimeanza
kutoa huduma kuanzia Jumamosi ya wiki iliyopita ya tarehe 15 ya mwezi
huu kama ilivyobainisha kupitia vyombo vya Habari.
Safari hizo zilianza kwa kutoa
huduma ya kusafirisha abiria kuelekea nchini Comoro na hapa nchini itoa
safari katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Kigoma.
Bi.Fungamtama amesema kwa kuanzia
walianza na mazoezi ya vitendo kwa marubani na wafanyakazi wa ndani ya
Ndege ambapo hatimaye walianza safari za biashara ya kusafirisha abiria
mnamo tarehe 15 Oktoba kama ilivyopangwa.
Ameongeza kuwa ATCL imeboresha
huduma zake kwa kiasi kikubwa kwa kuwapatia wateja wake ofa ya kubeba
kilo 20 za mizigo na kilo 7 za mzigo wa mkononi bure pamoja na kutoa
vinywaji na ubadilishaji wa tiketi ni bure ndani ya mwezi.
Aidha, Kaimu Afisa Mawasiliano wa Kampuni Bi.Lily amekanusha taarifa potofu kuwa zimekwama kuanza safari zilizopangwa.
Amesema kuwa habari hizo sio za kweli kwani hivi sasa wameshaanza huduma katika mikoa hiyo mitatu.
Kampuni ya Ndege ya ATCL kwa sasa
ina ndege tatu,zikiwemo mbili aina ya Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba
abiria 76 kila moja na Dash8-Q300 moja yenye uwezo wa kubeba abiria 50.
No comments:
Post a Comment