Thursday, 21 July 2016

Uchu wa madaraka chanzo cha vita vinavyoendelea Sudani Kusini

Ni nani aliyechochea mapigano ya karibuni huko Sudan Kusini yalioanza Ijumaa, Julai 8, yaliyosababisha zaidi ya watu 300 kuuawa na nchi hiyo changa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki?
Hilo ni swali linaloulizwa na watu wa nchi hiyo na pia na jamii ya kimataifa. Aprili mwaka huu Rais wa nchi hiyo, Salva kiir na makamu wake, Riek Machar, waliunda Serikali ya mpito baada ya kufikia mapatano ya amani mwaka mmoja uliopita.


Mapatano hayo yalisitisha vita vya kienyeji vilivyochomoza miaka mitano baada ya Sudan Kusini kujitenga kutoka Sudan.

Kwa nini Kiir na Machar wanagombana tena mara hii? Jibu ni kwamba Kiir anataka kubakia kuwa rais wa nchi, lakini Machar ana tamaa.

Kiir na Machar wanawakilisha makabila mawili makubwa katika Sudan Kusini, Wadinka na Wanuer, ambayo yamekuwa yakihasimiana kwa muda mrefu.

Mapigano yaliyoanza Desemba 2013. Mapigano ya karibuni ni kwamba mara kadhaa lilichomoza jina la mtu watatu: Paul Malong, Mkuu wa Majeshi ya Sudan Kusini ambaye ni mtu mwenye siasa kali za ukabila wa Kidinka na anapigania kabila lipate nafasi katika nchi hiyo.

Kwa hakika, Malong anataka aonekane kuwa ndiye hasa mwenye mamlaka nyuma ya kiti cha Kiir.

Kwa siku kadhaa kumekuwako mivutano katika mji mkuu wa Juba baina ya wapiganaji wanaomuunga mkono Machar na wanajeshi wa Kiir.

Machar aliporejea Juba kutoka mafichoni na uhamishoni, kama vile mapatano ya amani yalivyotaka, aliruhusiwa kuwa na wapiganaji wake 2, 000 katika mji huo. Wengi wa askari 10, 000 wa jeshi la Taifa waliwekwa kilomita 25 nje ya mji huo.

Hali hiyo ilikuwa ya hatari kwa wapiganaji wa Machar, bila ya shaka. Pale mvutano ulipozidi, Kiir na Machar walikutana katika Kasri la Rais kuujadili mzozo huo.

Mtu muhimu aliyekosekana katika mazungumzo hayo alikuwa Malong, licha ya kwamba kuwako kwake, kama mkuu wa majeshi, kulikuwa ni jambo la lazima.

Malongo anaweka kwamba hayatilii maanani mapatano ya amani yaliofikiwa baina ya Kiir na Machar. Anahisi Kiir amesalimu amri na amelegeza kamba katika masuala mengi.

Mkuu huyo wa majeshi anaonekana kama vile anahisi Sudan Kusini ni mali ya Wadinka, hivyo ni lazima watu wa kabila hilo wadhibiti nyadhifa muhimu katika Serikali, siasa na jeshi.

Anapowataja Wadinka anakusudia Wadinka wa Mkoa wa Bahr el-Ghazal ambako yeye na Kiir wanatokea na anaowaona kuwa ni bora kuliko wale wa maeneo mengine ya nchi.

Malong hajapendezwa na Serikali ya mpito iliyoundwa na ambayo ndani yake kuna watu wa mkabila mengine pia. Pia, hajavutiwa na wazo la kuwachanganya wanajeshi pamoja na wapiganaji wa Machar ili liundwe Jeshi moja la Taifa.

Kabla ya mwaka 2013 Wanuer walikuwa ni sehemu kubwa jeshini, lakini tangu vita vya kikabila kuanza Jeshi la Serikali limegeuka kuwa na Wadinka wengi.

Malong anataka urais
Tetesi zinaenea huko Sudan Kusini kwamba Malong anajaribu kuwagonganisha Kiir na Machar ili yeye aje kuwa rais. Kuna watu nchini humo wanaomuogopa Malong na kuna wale wanaomtuhumu, japokuwa hamna ushihidi uliotolewa hadi sasa, kwamba alikuwa dhamana ya mauaji ya Wanuer katika mji wa Juba pale vita vya kienyeji vilipoanza mwaka 2013.

Licha ya yote hayo bado haifahamiki nani hasa aliyesababisha mapigano ya hivi karibuni. Japokuwa mara hii, kama ilivyokuwa hapo kabla, jina la Malong limeibuka hapa na pale, lakini mambo mengi bado si wazi.

Pia mara hii, kama ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita, mapigano haya hajazuka papo kwa papo. Wakati ule, kama ilivyokuwa mara hii, lazima kulikuwako mpango ulioandaliwa kabla.

Amani imetoweka
Jambo moja ni hakika, nalo ni kwamba mpango wa amani wa Sudan Kusini kwa sasa umetupwa ndani ya pipa la taka. Baada ya kutokea mara hii mauaji mengine chuki zimeongezeka na hali ya kutoaminiana imezagaa. Amani kamili kwa sasa ni ndoto.

Mapigano haya ya karibuni huko Juba yameirejesha Sudan Kusini ndani ya janga jipya. Wote wawili, Kiir na makamu wake , Machar, hawajaijenga na kuipatia maendeleo nchi yao tangu iliopoata uhuru miaka mitano iliyopita.

Viongozi hao wawili wamejidhihirisha kwamba ni wababe katika kuendesha vita baina yao. Tatizo la Sudan Kusini ni tu uchu wa madaraka. Mahasimu hao wanataka wao na makabila yao wajilimbikizie madaraka. Jambo la ajabu na kusikitisha ni kwamba kila mmoja wao anahisi ana haki miliki ya kuogoza nchi na makabila mengine yawe mashahidi wa sarakasi yao.

Sumu hii ya ukabila ndiyo kiini cha mzozo wa Sudan Kusini. Sasa mapatano ya amani yaliyofikiwa Agosti mwaka jana na yaliyokomesha vita vya kienyeji vilivyochukuwa maisha ya watu 50, 000 hayana thamani yoyote.

Licha ya kwamba wote wawili, Kiir na Machar, waliweka alama za vidole vyao katika karatasi za mkataba huo, lakini kila mtu duniani alianza kuwa na wasiwasi pale Kiir tangu mwanzo alipoanza kuukosoa mkataba huo. Ishara ya kukosekana nia safi ya kuutekeleza mkataba huo ilionekana tangu mwanzo. Lakini walimwengu, kwa masikitiko, walilipuuza jambo hilo.

Uchumi umezorota
Licha ya uhasama baina ya Kiir na Machar, Sudan Kusini ina tatizo jingine kubwa tangu kupata uhuru, nalo ni la kiuchumi. Japokuwa Sudan Kusini ina robo tatu ya akiba ya mafuta yaliokuwako katika ardhi ya Sudan nzima, lakini Sudan Kusini hiyo inaitegemea Sudan Kaskazini kuweza kusafirisha mafuta yake kwenda ng’ambo.

Kwa miaka sasa Juba na Khartoum zimekuwa zikibishana vikali juu ya malipo ya kutumia mabomba ya kupitishia mafuta kutokea Sudan Kusini hadi Kaskazini na kuwasili bandarini katika Bahari ya Sham.

Mara kadhaa kumekuwako mapigano katika mpaka baina ya Sudan na Sudan Kusini. Pia, mambo yamekuwa magumu kwa Wasudani Kusini kutokana na kuporomoka bei ya mafuta katika masoko ya dunia, maisha kuwa ghali na ufisadi kuzidi nchini humo.

Suluhisho?
Sudani Kusini itakuwa katika hali bora ikiwa Kiir na Machar watastaafu na kuchukua pensheni zao. Lakini isisahaulike kwamba wao ni wawakilishi wa makabila mawili makubwa katika nchi hiyo.

Ama sivyo inawabidi wajifunze kuishi pamoja na kuheshimiana. Matarajio yako kwa Umoja wa Afrika (AU) na nchi zinazoizunguka Sudan, hasa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Itasikitisha pindi mzozo huu wa Kiafrika utawachiwa upatiwe ufumbuzi na madola makuu, nje ya Afrika. Pia, kuna nchi kadhaa duniani zilizokwenda mbio hapo zamani kuitia moyo Sudan Kusini ijitenge kutoka Sudan. Inafaa sasa nchi hizo nazo pia ziende mbio kuhakikisha Sudan Kusini ina angalau amani.

No comments:

Post a Comment