Friday, 22 July 2016
maduka 160 ya biashara yaliyopo eneo la Buzuruga katika manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza yamefungwa kwa saa 48
Zaidi ya maduka 160 ya biashara yaliyopo eneo la Buzuruga katika manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza yamefungwa kwa saa 48 na baada ya muda huo kumalizika, maduka hayo yatagawiwa kwa wafanyabiashara wengine, ambao watakuwa tayari kulipia kodi ya pango ya shilingi laki mbili kila mwezi kwa miezi mitatu mfululizo.
Maduka hayo yamefungwa hii leo asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi na askari mgambo wa manispaa hiyo, ambapo zoezi hilo limeongozwa na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela John Wanga.
Baadhi ya wafanyabiashara walioshindwa kulipia ongezeko la kodi ya pango baada ya kupewa notisi ya siku saba kuanzia julai 14 hawakuwa tayari kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hilo ambalo ni endelevu.
Kituo kikuu cha mabasi cha Buzuruga kina jumla ya maduka 213 na kati hayo ni maduka 49 tu ndio yametimiza masharti ya kulipa malipo ya shilingi laki mbili kwa kila mwezi kwa miezi mitatu mfululizo kwa hiyari.
Halmashauri ya manispaa ya Ilemela ilitoa notisi ya siku saba ya kuwataka wafanyabiashara kuondoa mali zao katika maduka na vibanda vinavyomilikiwa na halmashauri hiyo, baada ya kushindwa kutekeleza makubaliano ya kulipa kodi ya pango ya miezi mitatumitatu kuazia Julai mosi hadi Septemba 30 mwaka huu.
Kabla ya ongezeko hilo jipya la shilingi laki mbili, wafanyabiashara hao walikuwa wakilipa kodi ya shilingi elfu ishirini kwa kila mwezi.
Labels:
MWANZO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment