Saturday, 23 July 2016

Jinsi jina la kauzu fc lilivyotokea


 Na Kalonga Kasati
 
 umekuwa unajiuliza maswali mengi kuhusu timu ya Kauzu FC, kwanini imepewa jina hilo na lina maana gani lakini maswali yako yakakosa majibu.
Sasa Chief wa Kauzu FC imekuja na majibu ya maswali hayo ikiwa ni pamoja na maana halisi ya ‘Kauzu’ na kwanini waliamua kuiita timu yao jina hilo.
Katika stori mbili tatu na Sports Extra, Chief wa Kauzu akaeleza kwa undani juu ya jina Kauzu lilipotoka na maana yake halisi.


“Jina la Kauzu limetoka mbali sana, halijaja tu kirahisi na lina histori yake. Jina hili limetoka hapa kijiweni kwetu, wakati masela tunakutana na kukaa hapa kupiga stori, kulikuwa na mti wa mwarobaini (anauonesha) ulikuwa mdogo siyo kama unavyouona. Mti huu umepata shida sana na umepitia misukosuko mingi hadi umekuwa mkubwa namna hii,” amesema Chief wa Kauzu baada ya kuombwa fafanue kwanini timu yao inaitwa Kauzu jina ambalo kwa watu wengine limekuwa ni msamiati mpya.

“Mti huu ulikuwa unakojolewa na unavunjwa na kumwagiwa uchafu wa kila aina lakini ukakua kibishi. Kuanzia hapo tukawa tunauita ‘Mwarobaini Kauzu’.  Sababu ya kuuita mwarobaini kauzu ni kutokana na wale dagaa wa Mwanza ambao ni maarufu kwa jina la Kauzu (wabishi) hata wakipikwa bado watakuwa wametoa macho,” alindelea kueleza shabiki huyo ambaye umaarufu wake unakua kila kukicha kutokana na ubunifu wake katika kuishangilia timu yake.

“Kutokana na mti huu ulivyokua kibishi tukaupa jina la Kauzu tukiufananisha na wale dagaa wabishi, na tangu wakati huo eneo hili likawa linafahamika kwa jina la Mwarobaini Kauzu.”

“Tulipoanzisha timu yetu ya mtaani, tukawa tunahangaika kuipa jina ambalo litatutambulisha sisi na eneo letu. Kwasababu timu hii ilianzishwa na vijana ambao chimbuko lake ni hapa kwenye maskani ya Mwarobaini Kauzu, moja kwa moja tukaamua kuipa timu yatu jina ka Kauzu FC.”

Kuzu itacheza mechi yake ya nusu fainali Jumapili Julai 24 dhidi ya Misosi lakini leo kuna pambano kali kati ya Temeke Market dhidi ya Makumba FC mechi zote zinapigwa kwenye uwanja wa Bandari, Tandika lakini pia zinarushwa moja kwa moja kupitia Azam TV. Mwanaspoti wanaendelea kutoa zawadi kwa kila mchezaji bora wa kila mechi, kikundi bora cha ushangiliaji cha kila wiki na timu bora ya kila wiki huku Dr. Mwaka yeye ndiyo akisimamia show nzima ya Ndondo.

No comments:

Post a Comment