Tuesday, 24 May 2016

Twanga Pepeta kuzindua Albamu ya 13 Mwanza Jumamosi,


indexMkurugenzi wa bendi ya African Stars, Asha Baraka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  kuhusiana na uzindua albamu yake ya 13 ijulikanayo kwa jina la (Usiyaogope Maisha) mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park Jumamosi Mei 28.
 

Na Chrispino Mpinge
 
Bendi ya muziki ya African Stars “Twanga Pepeta” itazindua albamu yake ya 13 ijulikanayo kwa jina la Usiyaogope Maisha mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park Jumamosi.
Akizungumza jijini , Mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka alisema kuwa maandalizi ya uzinduzi huo yamekwisha kamilika na wanamuziki wake wapo kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya uzinduzi huo.
 
Mbali ya wimbo wa Husiyaogope  Maisha uliotungwa na Ali Choki, nyimbo nyingine zinazounda albamu hiyo ni Ndoa (Luizer Mbutu), Uso Chini, (Choki), Michepuko (Msafiri Diouf), Mapenzi Yanaumiza (Haji Ramadhani) na Ganda la Mua uliotungwa na Saleh Kupaza ambaye kwa sasa hayupo kwenye bendi hiyo.
 
Asha alisema kuwa wamekwisha rekodi nyimbo zote na mauzo ya CD 1000 ya kwanza, yatatumika kuchangia ununuzi wa madawati mkoani humo. Alisema kila CD itauzwa Sh3, 000 na Sh 1,000 watatumia kununua madawati.
 
 “Hii ni heshima kwa wapenzi wa muziki wa Mwanza, bendi inafanya uzinduzi wa albamu hii kwa mara ya kwanza mkoani, albamu zote 12 zilizinduliwa  hapa Dar es Salaam, hii ni mara ya kwanza katika historia ya bendi yetu,”
 
“Tunataka tuwe tofauti, mpango wa kununua madawati pia utafanyika katika uzinduzi wa albamu hiyo kwa mkoa wa Dar es Salaam katika siku itakayopangwa, tumepiga hesabu na kujua dawati moja ni Sh50,000 (kama utatengeneza mwenyewe), “ alisema Asha.
 
Alisema kuwa albamu hii ni ya aina yake kwani wanamuziki wake wametunga nyimbo ambazo mbali ya kuburudisha, pia zinatoa mafundisho mbalimbali.
 
Albamu za nyuma ya bendi hiyo ni  Kisa Cha Mpemba, Jirani, Fainali Uzeeni, Chuki Binfasi, Ukubwa Jiwe, Mtu Pesa,  Safari 2005, Password, Mtaa wa Kwanza, Mwana Dar es Salaam, Dunia Daraja na Nyumbani ni Nyumbani.
 Mwisho….
Caption:
Mkurugenzi wa bendi ya African Stars, Asha Baraka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  kuhusiana na uzindua albamu yake ya 13 ijulikanayo kwa jina la Husiyaogope Maisha mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park Jumamosi Mei 28.

No comments:

Post a Comment