Na Golden Mwakatobe
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL)
inatarajia kuanza kutoa huduma ya uuzaji wa tiketi kwa abiria wanaotumia
usafiri wa treni kwa mfumo wa kielektroniki lengo likiwa ni kuwawezesha
wananchi kuweza kurahisha ununuaji wa tiketi hizo na kupunguza
usumbufu.
Kauli hiyo imetolewa
na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame
Mbarawa wakati akijibu swali la nyongeza lililoihusu Wizara yake ambapo
ametaja maeneo ambayo mfumo huo utaanza kufanya kazi ni pamoja na Mpanda
mpaka Tabora, Kigoma mpaka Tabora.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mhandisi Edwin Ngonyani akijibu swali la
Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Sabreen Hamza lililotaka kujua kwanini TRL
isianzishe mfumo wa uwakala wa tiketi ili kupunguza adha wanayoipata
wakazi alisema kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri wa treni
katika Mikoa ya Kigoma, uuzaji wa tiketi katika Stesheni ya Reli Kigoma
umekuwa na changamoto kubwa kutokana na ulanguzi wa tiketi.
Amefafanua kuwa, ili
kudhibiti ulanguzi huo, Kampuni ya Reli Tanzania iliamua kubadilisha
utaratibu kwa kuuza tiketi siku za safari na kwa kutumia vitambulisho
jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ulanguzi wa tiketi
hizo.
Ameongeza kuwa,
utaratibu huo umekuwa na changamoto zake kwa kusababisha wasafiri kulala
stesheni au kuwalazimu kuamka alfajiri ili kuwahi tiketi hizo.
“Ufumbuzi wa kudumu wa
tatizo hili si kuanzisha mfumo wa uwakala ambao utaiongezea TRL gharama
za uendeshaji, tatizo kubwa lililopo ni idadi ndogo ya safari za treni
ambapo huduma inayotolewa hivi sasa haikidhi mahitaji halisi ya wananchi
na hivyo kuwa na uhaba wa tiketi kwa abiria”, alisema Mhe. Ngonyani.
Aliongeza kuwa ili
kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatarajia kuongeza idadi ya
treni za abiria kwa njia ya Kigoma ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa
Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment