Saturday, 21 May 2016

Mashindano ya kombe la Mkuu wa Majeshi ya ulinzi kufunguliwa rasmi 24 Mei mwaka huu









Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa ya ufunguzi wa mashindano ya kombe la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF CUP) ambayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 24 Mei 2016 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. Mgeni rasmi katika ufunguzi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe: Nape Nnauye.


 Mashindano haya yalianzishwa mwaka 2014, awali JWTZ lilikuwa likiteua wanamichezo wa kushiriki michezo ya kimataifa kupitia timu teule za Jeshi hali iliyopelekea kutovumbuliwa kwa vipaji vipya katika michezo, ikaonekana upo umuhimu wa kubadili mfumo wa uteuzi. Hivyo kuanzisha mashindano ya Kombe la  Mkuu wa Majeshi (CDF CUP) ambayo huanzia ngazi za vikosi hadi kufikia ngazi za brigedi.

lengo la mashindano haya ni kudumisha mshikamano, kuvumbua na kukuza vipaji, pia mashindano hayo yatatumika katika kuteua kombaini ya timu ya JWTZ itakayoliwakilisha Jeshi na Taifa kwa ujumla katika mashindano ya michezo ya majeshi na utamaduni kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika nchini Rwanda mwezi wa nane mwaka huu.

Kauli Mbiu ya mashindano haya ni “Michezo ni Ulinzi na Umoja Daima”
Timu zinazoshiriki mashindano haya ni Ngome (Makao Makuu JWTZ), Kamandi ya Jeshi la nchi kavu ikiwakilishwa na timu za Tembo, Faru, Nyuki, Mbuni na Chui, Kamandi ya Jeshi la Anga, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).

Mashindano haya yatahusisha michezo ifuatayo, Mpira wa miguu kwa wanaume, Mpira wa kikapu kwa  wanaume, Mpira wa mikono kwa wanaume, Mpira wa pete kwa wanawake na Mbio za nyika kwa wanaume na wanawake.Michezo hii itafanyika katika viwanja vya Twalipo vilivyopo Mgulani pamoja na uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Mashindano haya yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 06 Juni 2016. Mgeni rasmi katika ufungwaji wa mashindano haya anatarajiwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange.
Wananchi wote wanakaribishwa hakuna kiingilio.
Imetolewa  na  Kurugenzi  ya  Habari  na  Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P  9203,   Dar es Salaam,  Tanzania.

No comments:

Post a Comment