Wakati mwili wa aliyekuwa Mkuruenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson
Kabwe ukitarajiwa kuzikwa Jumatano ijayo kijijini wake Mamba, Mpinji
wilayani Same, chanzo cha kifo chake kimetajwa kuwa ni saratani ya tezi
dume na kuharibika kwa ini.
Kabwe (pichani) alifariki dunia juzi
alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge Dar es
Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mauti hayo yamemkuta ikiwa ni siku 38 baada ya kusimamishwa kazi
hadharani na Rais John Magufuli kwa tuhuma za kuingia mikataba
iliyosababisha hasara ya zaidi ya Sh3 bilioni.
Mtoto wa marehemu, Geofrey Kabwe, alisema baba yake alianza kuugua maradhi ya tumbo Julai mwaka jana.
Alisema Ilipofika Desemba, alizidiwa na familia iliamua kumpeleka India kwa matibabu zaidi.
“Alipofika
India waligundua kuwa alipata hitilafu ndogo kwenye ini, hivyo
akafanyiwa upasuaji, madaktari India walisema chanzo cha tatizo hilo ni
dawa alizokuwa akitumia,” alisema Geofrey.
Alisema mwishoni mwa
Januari, mkurugenzi huyo alirejea nchini akiwa na afya njema na alianza
kwenda kazini Februari huku akihudhuria kliniki katika Hospitali ya
Apollo nchini India.
Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda, hali
yake kiafya ilianza kuzorota na ilifikia hatua familia ilitakiwa
kukutana ili kushauriana kuhusu hali hiyo.
“Wiki mbili
zilizopita nilipigiwa simu nikiwa Arusha nikaelezwa kwamba hali yake
kiafya siyo nzuri, tulimwona daktari wake na akabainika kuwa na
Pneumonia (homa ya mapafu), akapewa dawa na sindano,” alisema Geofrey na
kuongeza:
“Baadaye tulimpeleka TMJ kwa ajili ya kipimo cha CTScan, jana
mchana majibu yalitoka yakionyesha kuwa ini lilikuwa limeharibika na
tayari mwili ulikuwa umeanza kuvimba. Ilipofika saa mbili usiku hali
ilibadilika akawa anakoroma na saa tatu usiku akafariki dunia,” alisema
Geofrey.
Taarifa zilizopatika jana zimeeleza kuwa Kabwe amekuwa
nje ya ofisi yake tangu alipoanza matibabu na siku ya kwanza kurejea
kazini ilikuwa Aprili 19 ambako alikutana na rungu la Rais John
Magufuli.
Msemaji wa familia, Dk Ez Machuve alisema
mipango ya mazishi inaendelea: “Atasafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani
kwake Jumanne jioni baada ya kuagwa hapa nyumbani kwake. Mazishi
tunatarajia kufanya kijijini Mamba Mpinji Jumatano.”
Meya wa
Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema katika kipindi chake cha
kufanya kazi, hakubahatika kushiriki kazi yoyote na Kabwe kutokana na
hali yake kiafya.
“Sikubahatika kufanya naye kazi, baada ya Rais kufanya
uamuzi mgumu, aliondoka hivyo sikuwahi kushiriki naye,” alisema Mwita.
Kilichomwondoa
kazini
Makosa yaliyosababisha Kabwe kusimamishwa kazi ni madai ya
kusaini mkataba kwa kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari
yanayotoka kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) Sh4,000 huku
akidaiwa kusaini mkataba mwingine wa Sh8,000 chini ya sheria ndogo ya
mwaka 2009.
Pia, madai ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa UBT
hasa kwenye utaratibu wa kutoa magari na kukodisha vyumba vya kupangisha
kinyume na taratibu na kuongeza muda wa mzabuni iliyeingia mkataba na
jiji wa maegesho ya magari kinyume na taratibu.
No comments:
Post a Comment