Na Chrispino Mpinge
Shirika
la Koyo la kutoka Japan limepania kuwekeza kwenye miundombinu ya umeme
wa gesi asilia na umeme jua ili kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi
waishio vijijini.
Hayo yamesemwa jana jioni (Jumatatu, Mei 9, 2016) na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa shirika la Koyo, Bw. Norio Shoji wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Tumepanga
kuwekeza kwenye maeneo matano ambayo mojawapo ni kujenga mtambo wa
kuchakata gesi kwa kutumia gesi asilia inayozalishwa hapa nchini. Mtambo
huu utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 1,000 za umeme,” alisema.
“Pia
tunao mpango wa kujenga mitambo ya umemejua inayoweza kujiunganisha
kwenye gridi (on-grid/off grid solar power plants) kwa ajili ya maeneo
vijijini na yale yasiyofikika kwa urahisi zaidi ikiwa ni pamoja na
kuboresha mfumo wa usambazaji umeme kwenye gridi ya Taifa ili Tanzania
iweze kuzalisha zaidi nishati hiyo na kuiuza nchi jirani,” aliongeza.
Bw.
Shoji alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana nia ya kuwekeza pia katika
sekta nyingine kama kilimo, sayansi ya tiba (medical science),
usafishaji na uyeyushaji madini (refinery-smelting), uzalishaji wa
bidhaa za viwandani na teknohama.
Akifafanua
zaidi Bw. Shoji alisema shirika lake kwa kushirikiana na makampuni
mengine makubwa ya Japan pamoja na Serikali ya nchi hiyo wamedhamiria
kuwekeza kwenye miundombinu hiyo kwa sababu wanataka Tanzania iwe ni
kitovu (hub) cha uzalishaji na iweze kulisha nchi jirani katika SADC na
EAC.
Akitolea
mfano, Bw. Shoji alisema mbali na miradi mingine wanayotaka kuwekeza,
gharama za kuweka mtambo wa kuzalisha megawati 1,000 za umeme
hazitapungua kiasi cha dola za marekani bilioni moja (sawa na sh.
trilioni 2.2).
Waziri
Mkuu alimshukuru Bw. Shoji kwa nia yake aliyoionyesha na akamtaka
achague eneo mahsusi kwa sababu Tanzania inahitaji umeme wa kutosha
katika kutekeleza azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
“Serikali
ya awamu ya tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza
ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake. Tunahitaji
uwekezaji mkubwa kwenye nishati ya umeme katika mikoa ya Kusini, ya
Kaskazini, ya Magharibi na hata mikoa ya kati,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa
upande wake, Bw. Suleiman M. Nassor alisema shirika la Koyo litafanya
uwekezaji huo kwa kushirikiana na kampuni ya SSF Limited ambayo
inajihusisha na masuala ya nishati.
“Tunashirikiana na shirika la Koyo pamoja na Serikali ya Japan ili kuleta unafuu wa maisha kwa Watanzania wenzetu,” alisema Bw. Nassor.
No comments:
Post a Comment