Na Golden Mwakatobe
Serikali
imesema kuwa Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na ajali nyingi
za barabarani kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015
zilizosababisha vifo vya watu pamoja na majeruhi.
Taarifa hiyo
imetolewa leo bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni wakati akijibu swali la Mbunge wa
Biharamulo Magharibi Mhe. Oscar Rwegasira kuhusu kuongezeka kwa vifo
vitokanavyo na ajali za barabarani.
Kwa mujibu wa
takwimu zilizotolewa na Mhe. Masauni kwenye taarifa hiyo Jiji la Dar es
Salaam limeongoza kwa kuwa na ajali 18,506 kati ya ajali 46,539
zilizotokea nchi nzima kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015.
“Takwimu za
nchi nzima zinaonesha kuwa Mwaka 2013 zilitokea ajali 23,842
zilizosababisha vifo 4,002 na majeruhi 20,689. Mwaka 2014 zilitokea
ajali 14,360 zilizosababisha vifo 3,760 na majeruhi 14,530 na mwaka 2015
zilitokea ajali 8,337 zilizosababisha vifo 3,468 na majeruhi 9,383.”
alisema Masauni.
Mhe. Masauni
alieleza kuwa kwa mwaka 2013 Mkoa wa Kipolisi Kinondoni uliongoza kwa
kuwa na ajali zipatazo 6,589 ukifuatiwa na Mkoa wa Kipolisi Ilala
uliokuwa na ajali 3,464 wakati Mkoa wa Simiyu na Tanga kulikuwa na ajali
chache ambapo Simiyu zilitokea ajali 67 na Tanga ajali 96.
Mwaka 2014
Kinondoni na Ilala ziliongoza tena kwa kuwa na ajali 3,086 zilizotokea
Kinondoni na Ilala ajali 2,516 na mikoa iliyokuwa na ajali chache ni
Simiyu ajali 55 na Kagera ajali 29.
Aidha, Mhe.
Masauni alisema kuwa mwaka 2015 Mkoa wa Kipolisi Ilala uliongoza kwa
kuwa na ajali nyingi za barabarani ambapo ajali 2,516 zilitokea mkoani
humo ikifuatiwa na Temeke uliokuwa na ajali 1,420 wakati mikoa ya Rukwa
na Arusha ilikuwa na ajali chache.
Mhe. Masauni
alibainisha kuwa mfumo endelevu wa wazi uliopo wa kutoa takwimu hizo ni
kupitia taarifa za mwaka za Jeshi la Polisi (Polisi Annual Report)
ambapo kila mtanzania anaweza kupata taarifa hizo za ajali.
No comments:
Post a Comment