Serikali kupitia Wizara ya Nishati
na Madini, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) itatoa Ruzuku ya
jumla ya Shilingi Bilioni 7.481 kwa Wachimbaji Madini Wadogo 59 ambapo
kiwango cha juu cha Ruzuku kwa Kikundi/Mtu binafsi kikiwa ni Shilingi
Milioni 210.
Hafla ya utoaji wa Ruzuku hiyo
itafanyika siku ya Jumatatu , tarehe 16 Januari 2017, Mjini Mpanda
mkoani Katavi, Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb.).
Fedha za Ruzuku kwa kila Mnufaika,
zitatumika kununua vifaa vya kuchimbia au kuchenjulia madini ambapo
kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo, wanufaika hao watapata mafunzo kuhusu
matumizi sahihi ya ruzuku yatakayotolewa na Wizara ya Nishati na Madini
tarehe 15 Januari, 2017 Mjini Mpanda.
Miradi 59 itakayopata ruzuku hiyo,
ndiyo iliyoshinda kati ya miradi 592 ya uchimbaji madini mdogo
iliyokuwa kwenye ushindani.. Waombaji wengine ambao maombi yao
hayakushinda watajulishwa kwa Barua.
Wizara ya Nishati na Madini
ilianza mchujo wa kuwapata Washindi tangu Mwezi Julai 2016, kwa
kuwashirikisha , Viongozi wa Wachimbaji Madini Wadogo wa mikoani
(REMA’s),Viongozi wa Kitaifa (FEMATA) pamoja na Viongozi wa Wachimbaji
Madini Wanawake (TAWOMA).
Majina ya wanufaika wa Ruzuku awamu ya tatu pia yanapatikana kwenye Tovuti ya Wizara: www.mem.go.tz pamoja na Ofisi Za Madini Za Kanda.
Imetolewa na,
Prof. Justin W. Ntalikwa
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment