Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Msomba ( wa tano
kushoto, waliokaa mbele) akielezea majukumu ya shirika hilo katika
kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na
Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud
Talib aliyeambatana pamoja na ujumbe.
Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini
wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk Wellington
Hudson akieleza jambo katika kikao hicho.
Kaimu Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu
wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Venosa Ngowi
akielezea shughuli za utafiti zinavyofanyika katika shirika hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Msomba
(katikati) akisisitiza jambo katika kikao hicho.
Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib (kulia) akifuatilia maelezo
yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo (hayupo pichani).
Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo (katikati, waliokaa mbele) na Waziri wa Ardhi,
Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib ( wa pili
kutoka kushoto, waliokaa mbele wakiwa katika picha ya pamoja na
watendaji kutoka Wizara husika.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Wizara ya Nishati na Madini kwa
kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar
zinatarajia kuunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuandaa Mpango wa
ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta za gesi na
mafuta.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki
na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika kikao
chake na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama
Aboud Talib aliyeambatana na Ujumbe wake.
Wengine waliohudhuria kikao hicho
ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa
Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli
za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA).
Profesa Muhongo alisema lengo la
kamati hiyo ni kujadili maeneo ya kushirikiana pamoja na kubadilishana
uzoefu katika sekta za gesi na mafuta
Alisema kuwa, kamati hiyo
itashirikisha Wataalam kutoka katika taasisi za Sheria, Ardhi, Kodi,
Gesi na Mafuta chini ya Makatibu Wakuu wa sekta husika kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar.
Waziri Muhongo alisema kuwa, uwepo
wa kamati hiyo utachochea Zanzibar kuwa na taasisi kama TPDC na
nyingine hivyo kupelekea ukuaji wa sekta ya gesi na mafuta.
Alisisitiza kuwa, Serikali ya
Tanzania Bara kupitia Wizara ya Nishati na Madini ipo tayari
kushirikiana na Serikali ya Zanzibar pamoja na kubadilishana uzoefu
katika masuala ya gesi na mafuta.
Profesa Muhongo alishauri
Serikali ya Zanzibar kuandaa wataalam wa mafuta na gesi kwa
kuwasomesha katika ngazi za diploma na shahada katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).
Akiongeza kuwa, Serikali ipo
tayari kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa Zanzibar wanaofanya vizuri
katika masomo ya Sayansi kwa ajili ya kusomea shahada ya uzamili
katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.
Naye Waziri wa Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib, alimshukuru Waziri
Muhongo kwa utayari wa Wizara ya Nishati na Madini katika kushirikiana
na Wizara yake kwenye shughuli za mafuta na gesi
Alisema kuwa, kamati itakayoundwa
itapelekea mambo kwenda kwa kasi na kuwa na data za pamoja zinazotokana
na utafiti wa mafuta na gesi na kupanga Mikakati ya kuvutia wawekezaji
kutoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment