Na. Aron Msigwa – NEC
Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imewataka wagombea na Vyama vya Siasa vinavyoendelea na kampeni za
Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Madiwani kufanya kampeni za kistaarabu
zinazozingatia maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 na kwamba Chama au
mgombea atakayekiuka maadili hayo atachukuliwa hatua.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mkuu (Mst. Znz.) Hamid M.
Hamid zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi huo
Januari 22, 2017 kufuatia baadhi Vyama na Wagombea kuanza kukiuka
Maadili na taratibu za Kampeni kwa kutoa matamko yaliyo nje ya Sera za
Vyama vyao.
Amesema kipengele cha 2.1 (m) cha
Maadili ya Uchaguzi kinachoeleza Wajibu wa Vyama vya Siasa na Wagombea
katika kuendesha shughuli za Siasa wakati wa Kampeni kinavitaka Vyama
vya Siasa, Wagombea na Wafuasi wao kufanya kampeni kwa kuzingatia
misingi inayolenga kutangaza Sera ambazo hazijengi chuki, mafarakano na
kuleta mgawanyiko katika jamii.
“Katika Kampeni zinazoendelea,
baadhi ya vyama vya Siasa vimeanza kukiuka taratibu za kampeni na
maadili na kutumia fursa ya kampeni vibaya, vinawasema viongozi wa
Kitaifa , kutoa matamko ambayo kihalisia siyo ya kumnadi mgombea na
kufanya kampeni zisizo za kistaarabu,” Amesema Jaji Hamid.
Amesema kuwa vyama Vyama au
Wagombea watakaoendelea kukiuka Maadili ya Uchaguzi katika Mikutano ya
kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Tanzania pamoja na
Jimbo la Dimani, Zanzibar watachukuliwa hatua.
Jaji Hamid ameeleza kuwa
kipengele cha 5.3 cha Maadili ya Uchaguzi kinaeleza wazi kuwa Chama au
Mgombea atakayekiuka Maadili ya uchaguzi katika jimbo au Kata yenye
uchaguzi mdogo atafikishwa katika kamati ya maadili ya ngazi husika na
kuchukuliwa hatua stahiki.
Aidha, kipengele cha 5.10 cha
Maadili ya Uchaguzi yaliyokubaliwa na Vyama vyote vya Siasa kinafafanua
kuwa Kamati za Maadili ya uchaguzi ngazi ya Taifa, Jimbo na Kata katika
kushughulikia malalamiko na kutoa adhabu zinaweza kuchukua hatua
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukitaka Chama au Mgombea kusahihisha kosa
au makosa au kuomba msamaha hadharani.
Hatua nyingine ni Kukisimamisha
Chama au Mgombea kuendelea kufanya kampeni za Uchaguzi, kutoza Faini,
Kutangaza jina la Chama au Mgombea aliyekiuka Maadili kwa kueleza kosa
au Makosa yake kupitia redio, televisheni, magazeti na njia nyingine za
mawasiliano.
No comments:
Post a Comment