Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali imetoa rai kwa wazazi
wote nchini kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa watoto ikiwemo
kuwapatia malezi bora na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili ili
waweze kukua vyema na kulisaidia taifa hapo baadae.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sihaba
Nkinga wakati akizungumza kwenye kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa
na kituo cha Televisheni TBC 1.
Nkinga alisema kuwa ni jukumu la
wazazi au walezi kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yote ya msingi
kama vile chakula, malazi, elimu pamoja na ulinzi ili waweze kuwa salama
katika mazingira wanayoishi na yanayowazunguka.
“Mzazi au mlezi anapaswa
kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mtoto na kumlinda dhidi ya ukatili
kwani imebainika kuwa kwa kiasi kikubwa ukatili wa watoto unaanzia
kwenye familia.” Alifafanua Nkinga.
Aidha amewataka baadhi ya
wanajamii kuacha kumaliza kesi za ukatili kwenye ngazi ya familia badala
yake watoe taarifa polisi pindi watoto wanapofanyiwa vitendo vya
ukatili iwe kupigwa, kubakwa au kulawitiwa ili wahusika waweze
kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Alieleza kuwa kwa mwaka 2016 kuna
ongezeko la asilimia 31 kwenye utoaji taarifa za matukio ya ukatili kwa
watoto lakini bado uhamasishaji unaendelea ili matukio yote yawe
yanaripotiwa na sheria ichukue mkondo wake.
“Wazazi wawe wanatoa taarifa
haraka kwenye vyombo husika kwani matukio ya ukatili kwa watoto
yanawaathiri kiafya, kisaikolojia na hata kupelekea vifo.”
Akizungumzia juhudi za Serikali,
Nkinga alisema kuwa jitihada mbalimbali zinafanyika kukomesha ukatili
kwa watoto na Serikali inafanya mapitio ya baadhi ya kanuni za Sheria ya
Mtoto ya mwaka 2009 ambazo zimepitwa na wakati.
Akifafanua kuhusu Mpango wa
Kitaifa wa Kudhibiti Ukatili wa Watoto na Wanawake uliozinduliwa mwaka
2016 alisema umelenga kuwapatia elimu watoto wa kike na Serikali
itashirikiana na wadau wa elimu ili mtoto wa kike aweze kusoma katika
mazingira bora na salama.
Aidha Nkinga alisema kuwa pamoja
na uwepo wa Dawati Maalum la Watoto kwenye vituo vya Polisi, Serikali
ina mkakati wa kuweka Dawati la Ulinzi na Usalama katika shule za Msingi
na Sekondari kote nchini ili watoto waweze kupata elimu ya kujilinda na
kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.
No comments:
Post a Comment