Vanilla (Vanilla fragrans) asili yake ni Amerika ya kati huko Mexico, Guatemala na Costa Rica ambako ilianza kutumika tangu karne ya 15.
Zao la vanilla lilifika barani Ulaya karne ya 16, kisha likapelekwa visiwa vya Reunion, hatimaye kusambazwa Mauritius, Madagasca, Shelisheli, Tahiti na Comoro kati ya karne ya 18 na 19. Zao hili kwa sasa linazalishwa kwa wingi sehemu za Madagasca, Comoro na Reunion. Hapa Tanzania zao hili liliingizwa mkoani Kagera mwaka 1962 kutokea nchini Uganda.
Hata sasa Mkoa wa Kagera ndio unaozalisha zao hili katika wilaya za Bukoba na Muleba, na pia huko Zanzibar. Zao hili linaleta fedha za kigeni kwa nchi na kuleta ajira kwa wananchi. Vanilla ni zao ambalo hutumika kuongeza ladha katika vyakula na vinywaji vya aina mbalimbali. Matumizi makubwa ya zao hili ni kuongeza harufu nzuri na ladha ya vyakula na vinywaji mbalimbali.