Friday, 11 March 2016

Wilaya nne Zaungana kuendeleza Maeneo ya Utalii wa kijiolojia

olduvai
Na Nechi Makundi

Wilaya nne za Ngorongoro, Karatu,Monduli na Longido,mkoani Arusha, zimekubaliana kuingia katika mradi wa kitalii wa kuhifadhi na kuendeleza maeneo yenye urithi wa kijiolojia(Geopark).

Mradi huo, unaoratibiwa na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) unategemewa kuwa kivutio kikubwa cha watalii na watafiti na utasaidia pia kuendeleza jamii zilizo na maeneo hayo.

Mkurugenzi wa idara ya mambo ya kale, Donatus kamamba akizungumza katika semina ya kuanzisha mradi huo, ambayo ilishirikisha wakuu wa wilaya hizo na wenyeviti wa halmashauri, alisema mradi huo ukianza utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa.

Alisema mradi huo,utasaidia sana kuhifadhi rasilimali zote za kijiolojia, kihistoria na kitamaduni katika wilaya hizo hivyo kutoa fursa za ajira kwa wananchi.

Wakizungumzia mradi huo, Mkuu wa wilaya ya Longido Ernest Kahindi na Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro,Hashimu Mgandilwa walisema wanaimani wananchi wa wilaya zao kunufaika na mradi huo.
Kahindi alisema wilaya ya Longido, ambayo ina maeneo ya kijiolojia ambayo ni muhimu katika utalii, itaweza sasa kupata fedha za kigeni katika kuhifadhi maeneo hayo.

Kwa upande wake Mgandilwa alisema wilaya ya Ngorongoro yenye maeneo kama Mlima oldonyolengai,  inatarajiwa kunufaika kwani miradi itakuwa inasimamiwa na wananchi.

Mwenyeviti wa halmashauri ya Karatu, Jubilate Mnyenye na Mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli, Isack Joseph walisema mradi wa Geopark ni fursa mpya kwa wananchi.

Mnyenye alisema wilaya ya karatu ambayo ina maeneo menji ya urithi wa kijiolojia ziwa eyasi na mengine  sasa inatarajia kuendelezwa maeneo hayo.

kwa upande wake Mwenyekiti wa Monduli, alisema ni wazi fursa ya mradi wa Geopark ikitumiwa vyema ibadili masisha ya wananchi wake na kuongeza mapato kwa halmashauri.

Mratibu wa mradi huo Mhandisi Joshua Mwankunda alisema mradi huo, hutolewa na shirika la umoja wa mataifa la utamaduni    (UNESCO) baada ya  kukidhi vigezo vinavyotakiwa.

Alisema  baada ya kupata hadhi ya geopark maeneo hayo hujiunga na mtandao wa kidunia  wa maeneo ya Geopark na hivyo kuvutia watalii na watafiti.

No comments:

Post a Comment