Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali
Watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Victor Kimaro (katikati)
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo
jijini Dar es Salaam kuhusu kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa
kuwajengea uwezo wa kitaalam watumishi wa mamlaka hiyo ili kuongeza
makusanyo ya ndani , kushoto ni mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la
Japan (JICA) Toshio Nagase na kulia ni Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof.
Isaya Jairo.
Mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Japan (JICA) Toshio Nagase (kushoto) akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es
Salaam kuhusu kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa kuwajengea
uwezo wa kitaalam watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na
mkakati wa kuanza kwa awamu ya pili ya mradi huo, katikati ni Kaimu
Mkurugenzi wa Rasilimali TRA Bw. Victor Kimaro na kulia ni Mkuu wa Chuo
cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo.
Na. Kalonga Kasati
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamekamilisha awamu ya
kwanza ya kutoa mafunzo ya kuwajenga uwezo wafanyakazi wake ili
kuwawezesha kukabiliana na mabadiliko ya ukusanyaji kodi nchini.
Akizungumza na waandishi wa
habari mapema hii leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa
Rasilimali Watu wa Mamlaka hiyo Bw. Victor Kimaro amesema kuwa mafunzo
hayo yametolewa kwa ushirikiano wa TRA na Shirika la Maendeleo la Japan
(JICA) kwa muda wa miaka minne tangu Februari 2012 hadi Machi 2016.
“Kwa sasa wafanyakazi hawa
wataweza kuboresha mazingira ya ulipaji kodi ambayo huwa yanabadilika
kutokana na baadhi ya watu kukwepa kodi” alisema Bw. Kimaro..
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Kodi Profesa Isaya Jairo
amesema kuwa jumla ya Wafanyakazi 608 wa Mamlaka hiyo wamefaidika na
mafunzo hayo ambayo yamegharimu zaidi ya Dola za kimarekani milioni 3.5.
“Kwa sasa baada ya kukamilika kwa
mafunzo haya ya awamu ya kwanza, mamlaka itaweza kuongeza makusanyo ya
mapato kutokana na uwezo wa kiutaalam walioupata watumishi wa TRA”
alisema Prof. Jairo.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA, Bw. Toshio Nagase,
alisema Serikali ya Japan imekubali kuanza mradi mwingine wa ushirikiano
wa kitaalam kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ili kuendeleza
ushirikiano kati ya TRA na JICA.
Awamu ya pili ya mafunzo ya
kujenga uwezo wa kitaalam yanatarajiwa kuanza mwaka huu mara Baada ya
Makao Makuu ya Shirika la Maendeleo la Japan kumaliza kufanya uchambuzi
wa Maandalizi na kuchagua mbinu za utekelezaji wa mradi huo.
No comments:
Post a Comment