Na Chrispino Mpinge
MPANGO wa Kunusuru Kaya Masikini
Tanzania (TASAF III) umetoa zaidi ya shilingi Milioni 137.8 kwa kaya
masikini 3627 katika vijiji 57 wilayani Serengeti mkoani Mara.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa
TASAF Wilaya ya Serengeti Bi Nancy Nzota alipokuwa Akiongea na wananchi
wa kijiji cha Gesarya, Kata ya Rung’abure kuhusu malipo ya kaya hizo
kuwa yamefikia awamu ya tano.
Alisema Malipo ya fedha hizo yameyotolewa katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huo kwa mwezi Machi hadi Aprili 2016.
“Fedha hizi mnazopewa ni mbegu na
mnapaswa kuzitumia kukidhi mahitaji muhimu yakiwemo ya Elimu, afya na
kuanzisha shughuli za uzalishaji” alisema Bi Nancy.
Bi Nancy aliongeza kuwa,
watendaji wa vijiji wanatakiwa kubaini kaya zinazotumia fedha hizo
kinyume na matakwa ya mpango huo ambapo amewataka watendaji
watakaogunduliwa Waondolewe katika uwakilishi wa kaya na mchakato wa
kubadili wasimamizi/wawakilishi wapya Wa kaya zao ufanyike kwa utaratibu
maalumu.
Aliwaonya Wanufaika wa mpango huo
kutokutumia fedha hizo kwa shughuli zinazokinzana na Mpango huo kwani
kufanya hivyo hakutawatoa wananchi katika hali ya umasikini.
Alisema kuwa elimu hasa ya
ujasiriamali ilishatolewa kwa wanufaika katika kila kijiji juu ya
kuanzisha shughuli za ufugaji, kilimo na biashara ndogo ndogo.
Aliongeza kuwa pia elimu hiyo
huendelea kutolewa mara kwa kwa mara na wawezeshaji wa Mpango wa TASAF
ambao hutoa elimu hiyo kwa wananchi katika kila awamu ya malipo.
Mpango huu ulizinduliwa mkoani
Dodoma, Agosti 2012 na Rais mstaafu, Dk Jakaya Kikwete, Ambapo kwa
Wilaya ya Serengeti malipo kwa kaya masikini lilianza rasmi Julai 2015
na limeonesha kuanza kuzinufaisha kaya hizo.
No comments:
Post a Comment