Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akielkea kwenye soko la samaki la Feri akitokea
ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam kukagua hali ya soko hilo
Machi 22, 2016. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond
Mushi.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua eneo la kukaangia samaki kwenye soko la
samaki Feri la jijini Dar es salaam Machi 22, 2016, Kushoto kwake ni
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mama Lishe wakati alipotembelea
soko la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia Mama Lishe wakati alipotembelea
soko la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameiagiza Bodi ya soko la Kimataifa la Samaki la Feri, kukutana na
makampuni mbalimbali yanayouza gesi ili kupata kampuni inayouza kwa bei
nafuu Zaidi lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama wakaangaji wa samaki
sokoni hapo.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka
Meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi kuhakikisha Wanakuwa na kifaa
maalumu cha kupimia ujazo wa mitungi ya gesi sokoni hapo ili kubaini
kama ni sahihi.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko
la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa
majiko ya gesi sokoni hapo ambapo aliridhishwa na unavyofanya kazi.
Waziri Mkuu ambaye ametumia dakika
44 kulitembea soko hilo, alitoa maagizo hayo baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamesema wamekuwa wakiuziwa
gesi kwa bei kubwa ambayo imekuwa ikiongezeka mara kwa mara.
Akizungumza kwa niaba ya
wafanyabiashara hao, Bw. Ally Iddi amesema awali walikuwa Wanauziwa
mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 32 kwa sh. 70,000 na sasa umeongezeka
hadi sh. 98,000 kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na uzalishaji
wao. “Nimeulizia kwenye baadhi ya Maduka na kukuta mtungi wenye ujazo
kama huo unauzwa sh. 75,000,” alisema.
Kijana mwingine ambaye ni
mkaangaji wa samaki, Bw. Mwanya Selemeni alisema hivi sasa hali ya Soko
la feri ni nzuri tofauti na walivyokuwa wakitumia kuni kwa sababu hakuna
moshi. Alimuomba Waziri Mkuu ahakikishe wanafikishiwa gesi ya kutoka
Mtwara ili gharama ziweze kupungua.
Mfanyabiashara mwingine wa soko
hilo, Bi. Mariam Samweli ambaye alikuwa akiuza kuni na sasa Yeye na
wenzake wanataka kufanya biashara nyingine lakini banda walilokuwa
wakilitumia halina Umeme licha ya kuwa wameomba mara nyingi. “Tunaomba
kupatiwa umeme ili tuweke vipepeo tuweze kufanya biashara nyingine,”
alisema.
Waziri Mkuu pia alitembelea eneo
la mnada wa kuuza samaki sokoni hapo ambako alielezwa Matatizo ya umeme
na uzibaji wa mitaro ya maji machafu hali ambayo inatishia usalama wa
afya zao.
“Kuna jipu la umeme hapa,
tunachangishwa hela na kumpa mtu ambaye hatumjui lakini hatujawahi kuona
risiti, wao wanaweka umeme juu kwa juu na umeme wenyewe wala haukai.
Mita tunayo Hapa lakini hata namba hatujapewa,” alisema Bw. Omari Masoud
kwa niaba ya wenzake.
Kuhusu tatizo la uzibaji mitaro na
kutiririsha majitaka, kiongozi wa mama lishe sokoni hapo, Bi. Fatma
Ally aliomba watatuliwe tatizo hilo ambalo limedumu kwa zaidi miezi
miwili.
Akijibu kero zao, Waziri Mkuu
alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Raymond Mushi Asimamie Suala la
kuweka umeme kwenye hilo banda pamoja ahakikishe mama lishe wa soko hilo Upande wa mnadani waanze kutumia majiko ya gesi badala ya mkaa.
Kuhusu mitaro, alimwagiza meneja
wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi aimarishe uzibuaji wa mitaro katika soko
hilo. “ Mwambie mkandarasi azibue mitaro kila siku jioni na watumiaji
wa soko Waache kutumia mifuko ya plastiki kwa sababu inapoingia kule
inaziba na wala haiozi,” alisema.
Aliwataka wafanyabiashara
waimarishe usafi kwa sababu ni sehemu ya chakula. “Lengo letu ni Kufanya
soko hili liwe kwenye viwango vya kimataiafa ili mteja anapokuja
kununua samaki Wabichi ama wa kukaanga awe na chaguo,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa soko
hilo, Bw. Mushi alisema bodi ya soko hilo ambayo imeundwa Hivi karibuni
itakutana kesho kwa mara ya kwanza na miongoni mwa mambo
yatakayojadiliwa ni Maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
- L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016.
No comments:
Post a Comment