Na Kalonga Kasati
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC),imesema haitambui kujitoa kwa Chama cha Wananchi (CUF),katika Uchaguzi wa Mbunge Jimbo la Kijitoupele hapa Zanzibar unaotarajiwa
kufanyika Jumapili licha ya kuwa Tume imepokea barua rasmi toka kwa
uongozi wa Chama hicho.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya
Taifa Bw Kailima Ramadhani amesema Tume imefikia Maamuzi hayo kutokana
na ukweli kuwa barua hiyo ya CUF imechelewa huku maandalizi ya Uchaguzi
huo yakiwa yamekamilika na ni Wananchi tu kwa sasa Wanasubiriwa kwenda
kupiga kura.
Aidha Bw Kailima ameeleza
kuwa,kwa kuwa karatasi za kupigia kura zilishachapishwa na kuwasili Hapa
nchini tayari kwa uchaguzi huo,zitaendelea kuwa na picha za Wagombea wa
CUF hata kama wamejitoa katika uchaguzi huo.
Awali,wajumbe wa Tume ya Taifa ya
uchaguzi wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji mstaafu Hamid
Mahamood Hamid walitembelea katika vituo mbalimbali vya kupigia kura
katika Jimbo la Kijitoupele ili kujiridhisha na maandalizi ya uchaguzi
huo kabla ya uchaguzi kufanyika jumapili.
Tume ilibaini kuwepo kwa baadhi
ya kasoro ndogondogo katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ikiwa ni
pamoja na kubanduliwa kwa karatasi zenye majina ya wapiga kura,mfano
katika kituo cha Skuli ya sekondari Kinuni.
Jimbo la Kijitoupele lina jumla
ya Wapiga kura wapatao 17,274 na vituo vipatavyo 53 vitatumiwa Na wapiga
kura ili kumchagua mbunge wa Jimbo la Kijitoupele siku ya Jumapili.
Sambamba na Uchaguzi wa Ubunge
katika Jimbo la Kijitoupele, marudio ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba
25,2015 ambayo Matokeo yake yalifutwa uatafanyika Jumapili hiyo pia.
Uchaguzi katika jimbo la
Kijitoupele uliahirishwa mwaka jana kutokana na hitilafu ndogondogo Zilizojitokeza katika karatasi za kupigia kura,kabla ya kufutwa kwa
matokeo ya Uchaguzi Mkuu Wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25,2015.
No comments:
Post a Comment