Na Kalonga Kasati
Watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Temeke walioko masomoni na likizo wametakiwa kurudi ara moja
katika vituo vyao vya kazi ili kuhakikiwa.
Agizo hilo limetolewa hivi
karibuni na uongozi wa Halmashauri hiyo ikiwa ni katika kutekeleza Agizo
la Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli la kuhakiki watumishi wote wa umma
waliopo kwenye orodha ya malipo ya watumishi wa umma ndani ya siku 15
ili kubaini watumishi hewa wanaoendelea kulipwa mishahara.
Akizungumza kwa njia ya simu
msemaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Bi Joyce Nsumba Amesema zoezi
hilo ni muhimu sana kwa watumishi hivyo basi watumishi wote wa
Halmasahuri Hiyo waliopo likizo na masomoni wanatakiwa kurudi katika
vituo vyao vya kazi ili kuhakikiwa.
“ Taarifa imeshatoka kwa
watumishi wote kuwa wanatakiwa kuhakikiwa na kwa wale waliopo likizo na
kwenye masomo wanatakiwa kurudi ili wahakikiwe na kuendelea na likizo na
masomo Yao kwani mara baada ya uhakiki huu kukamili majina ambayo
yatakuwa hayajahakikiwa yatafutwa kwenye orodha ya watumishi” Alisema
Bi Joyce.
Bi Joyce Nsumba ameongeza kuwa
mpaka sasa uhakiki unaendelea kwa makundi mbalimbali Wakiwemo watumishi
kutoka Idara ya Afya, Elimu, Fedha na Biashara, Kilimo,Mifugo,Ujenzi,na
Maendeleo ya Jamii na mpaka sasa wameshahakiki zaidi ya watumishi
8,000.
Zoezi la uhakiki wa watumishi wa
umma nchini limekuja mara baada ya uchunguzi uliofanywa katika Mikoa ya
Singida na Dodoma katika Halmashauri 14 na kugundulika kwa watumishi
hewa 202 wanaolipwa mishahara na hivyo Mhe. Rais Magufuli kutoa agizo
la kuhakiki watumishi wote katika Wizara,mikoa,Wilaya,Idara,Taasisi na
Wakala za Serikali ndani ya siku 15.
No comments:
Post a Comment